Mtuhumiwa wa mauaji Mbeya auawa akiwakimbia polisi

HomeKitaifa

Mtuhumiwa wa mauaji Mbeya auawa akiwakimbia polisi

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeripoti kuwa mnamo Oktoba 16, 2026 katika Mtaa wa Makunguru, Kata ya Ruanda, mhudumu wa nyumba ya kulala wageni iitwayo Igogwe, Nice Kabuje alitoa taarifa polisi kuwa katika nyumba hiyo ya wageni imekutwa miili ya watu wawili jinsia ya kike ikiwa imefichwa uvunguni mwa kitanda.

Taarifa ya Polisi imesema baada ya kufika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, mwili mmoja ulitambulika kuwa ni wa Annastazia Mwakipesile (32) na mwingine bado haujatambuliwa mpaka sasa, na kwamba mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Aidha, polisi wamesema katika ufuatiliaji wa wahusika wa mauaji hayo, walifanikiwa kumshikilia Benson Steven maarufu kama Mkembo, fundi sofa na mkazi wa Iwambi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha matukio hayo ni imani za kishirikina kwa lengo la kupata utajiri kwani alieleza kabla ya kufanya kitendo alikwenda kwa mganga. Mtuhumiwa alikubali kwa hiari yake kuwaongoza askari hadi nyumbani kwa mganga wa jadi aliyempa masharti hayo ili apate utajiri,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Imeongeza kuwa wakiwa njiani wakielekea kwa mganga huyo, ghafla mtuhumiwa aliruka kutoka kwenye gari na kukimbia, hali iliyopelekea askari kufyatua risasi juu kwa lengo la kumzuia. Polisi wamesema baada ya mtuhumiwa kukaidi, askari alifyatua risasi iliyompata mguuni na kupelekea kifo chake wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Jeshi la Polisi limesema kumbukumbu zinaonesha kuwa mtuhumiwa aliwahi kukamatwa Temeke, Dar es Salaam na kushitakiwa kwa kosa la kuvunja nyumba na kuiba, ambapo alihukumiwa mwaka mmoja jela. Pia mwaka 2025 mkoani Mbeya alifikishwa mahakamani kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo aliachiwa huru baada ya mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani.

error: Content is protected !!