Baraza la Wawakilishi la Zanzibar limepitisha sheria mpya ya kuanzisha ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt Mwinyi Talib Haji amesema sheria hiyo itaongeza hadhi na utambulisho wa Mufti mkuu wa Zanzibar kama ilivyo katika nchi mbalimbali duniani.
Dkt. Talib amesema ulimwenguni kote Mufti Mkuu anapewa hadhi kubwa hivyo si vibaya Zanzibar ikiwa sehemu ya dunia inayotambua umuhimu wa kumpa cheo hicho badala kuitwa tu Mufti wa Zanzibar kama ilivyo sasa.
“Mtu anayewekwa katika nafasi hiyo lazima awe na hadhi kubwa kwani yeye ndio msemaji wa Waislamu akiwa ndani ya nchi na nje ya nchi,” amesema.
Sheria hiyo inahusisha vifungu vinavyoelekeza vigezo vya kumpata Mufti Mkuu wa Zanzibar, pamoja na majukumu yake.