Mbowe anaweza kufungwa miaka 15 jela

HomeKitaifa

Mbowe anaweza kufungwa miaka 15 jela

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu (Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya) wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo vya kigaidi.

Tumekuwekea baadhi ya dondoo kuhusu kesi ya ugaidi:

Ugaidi katika Sheria za Tanzania.
Mwaka 2002 Bunge la Tanzania lilitunga sheria ya kudhibiti na kupambana na ugaidi (Prevention of Terrorism Act (POTA)). Pamoja na mambo mengine, Sheria inatafsiri ugaidi kama uhalifu ambao unalenga kusababisha hofu kwa jamii, kushinikiza Serikali kufanya au kuachana na jambo fulani pamoja, kudhoofisha au kuharibu kabisa mifumo ya kisiasa, kikatiba, kiuchumi na kijamii katika nchi au jumuiya ya kimataifa. Hayo yameendeleza kwa upana kwenye kifungu namba 4 cha Sheria ya Kupambana na Ugaidi.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo (hususan kifungu namba 5), makosa ya ugaidi yanahusisha pia kupanga njama, kuongoza au kusaidia njama hizo, kushiriki mikutano yenye nia ya ugaidi, kutoa vifaa na mambo mengine yote yanayoweza kufanikisha ugaidi. Hivyo mtu anahesabika kuwa gaidi kwa kupanga, kutenda au kusaidia kwa ugaidi kwa namna yoyote ile.

Mbowe na wenzake.

Mbowe ni mshtakiwa wa 4 katika kesi hiyo. Wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa, kati Mei Mosi 2020 na Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha. Inadaiwa walikula njama za kulipua vituo mbalimbali vya mafuta na katika mikutano isiyokuwa ya kisiasa na kusababisha hofu kwa wananchi kwa lengo la kuutishia umma wa Tanzania.

Shitaka lingine ni kufadhili vitendo vya kigaidi, linalomkabili Mbowe ambapo anadaiwa katika tarehe hizo, katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, Mbowe aliwafadhili Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya, huku akijua ufadhili huo utatumikia katika kutekeleza vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo ya mafuta na mikusanyiko ya wananchi.

Hukumu.
Iwapo Freeman Mbowe na wenzake watakutwa na hatia katika mashtaka hayo, hukumu yake yaweza kuwa miaka isiyopungua 15 jela. Hiyo ni kwa sababu Sheria inaeleza kwamba mtu anyekutwa na hatia ya kutoa au kukusanya fedha kwa lengo la kufanikisha ugaidi, anastahili kiufungwa jela miaka 15-20. Kutoa au kukusanya mali, au kumkaribisha mtu atoe mali au kuweka mazingira ya uwepo wa mali au fedha na huduma zifananazo ili kufanikisha, adhabu yake sio chini ya miaka 20 jela.

Kesi ya Mbowe na wenzake itaunguruma tena Septemba 6, 2021 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mkoani Dar es Salaam.

error: Content is protected !!