Uamuzi pingamizi la Mbowe kutolewa leo

HomeKitaifa

Uamuzi pingamizi la Mbowe kutolewa leo

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu leo Septemba Mosi, 2021 wamefikishwa katika Makahama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumi Uchumi, kwa ajili ya kusikiliza maamuzi juu ya pingamizi walilowasilisha mahakamani hapo la kupinga kesi yao kusikilizwa na mahakama hiyo.

Agost 31, 2021 Mbowe na wenzake waliwasilisha pingamizi mahakamani hapo kupinga mahakama hiyo kusikiliza kesi yao kwa kuwa kulingana na Sheria ya Kuzuia Ugaidi mashitaka yao yanapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu na sio divisheni maalumu.

Baada ya washtakiwa hao kuwasilisha pingamizi hilo, Serikali imepinga hoja hizo ikidai kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 3 ya Mwaka 2016 makosa yaliyoko kwenye Sheria ya Ugaidi yaliwekwa kwenye Sheria ya Uhujumu Uchumi na kwamba kwa hali hiyo Mahakama ya Ufisadi ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yao.

Kutokana na hoja hizo, Jaji Elinaza Luvanda anayesikiliza shauri hilo, alipanga kutoa uamuzi leo.

Watu wachache tu ndiyo wameruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mahakama kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo, huku wengi wao wakisalia katika viwanja vya mahakama hiyo kutokana na tahadhari ya ugonjwa wa Uviko -19.

Katika kesi hiyo ya msingi namba 16/2021, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili pesa kwa ajili vitendo vya kigaidi.

error: Content is protected !!