MV Mwanza kufanya safari za Kenya na Uganda

HomeKitaifa

MV Mwanza kufanya safari za Kenya na Uganda

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema meli ya kisasa ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu itaanza kufanya safari za Uganda na Kenya katika ziwa Victoria baada ya ujenzi wake kukamilika.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 24, 2023 kuwa meli ya Mv. Victoria itaendelea kutumika kwa safari za Mwanza-Bukoba kupitia Kemondo na haitatumika kwa safari za Kenya, Uganda.

Akijibu swali la Mbunge wa Mleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), Naibu Waziri amesema meli hiyo ya Mv. Victoria kwa sasa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa ukanda huo.

Mwijage alihoji “ni lini Serikali itapeleka Meli ndogo ya abiria Muleba pamoja na kutumia meli ya MV. Victoria kujaribu masoko ya nchi za Uganda na Kenya?”

“Serikali inatambua hitaji kubwa la usafiri wa wananchi Wilayani Muleba, hususani waishio katika Visiwa. Kwa kutambua hitaji hilo, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imejenga meli moja MV. Claris kutoa huduma katika visiwa vya Godziba Wilayani Muleba na visiwa vya Gana Wilayani Ukerewe,” amesema Naibu Waziri.

“Meli hiyo iliyokuwa iliyoanza kutoa huduma katika visiwa hivyo Machi 3, 2023 ilisimama Machi 22, 2023 baada ya kupata hitilafu za kiufundi. Huduma hizo zitaendelea kuanzia mwanzoni mwa mwezi Mei, 2023 baada ya matengenezo kukamilika.”

error: Content is protected !!