Aliyeibuka kuwa Mwanafunzi bora kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba, Eluleki Haule ambaye alisoma shule ya St Anne Marie Academy ameahidiwa kusomeshwa bure kidato cha tano na sita na Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk Jasson Rweikiza wakati wa halfa iliyoandaliwa na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam ili kumpongeza kwa ushindi wake.
“Niwashukuru walimu kwani walipambana sana hadi kufanikiwa kupata mafanikio haya, pia nimshukuru Mkuu Wa Shule kwa uongozi bora pamoja na wanafunzi wote waliofanikiwa kufanya vizuri katika mitihani yao na niwasisitize muendelee kusoma kwa bidii kwani taifa linawategemea, “alisema Rweikiza.
Mbali na kumsomesha bure, shule hiyo itampa Sh milioni tatu, kumpeleka kumtambulisha bungeni Dodoma yeye na wazazi wake na kubandika picha yake kwenye magari yote 51 ya shule hiyo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James alimpongeza Eluleki na kumtaka aendelee kufanya vizuri kwenye masomo yake ya sekondari huku akisema matokeo hayo ni ishara kwamba wazazi na walimu wanatimiza majukumu yao huku akitoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kuwalea watoto katika maadili mema na kutoa kipaumbele kwenye elimu ili baadaye wajisaidie na kulisaidia taifa kwa ujumla.