Ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa yazaa matunda, wafanyabiashara wanufaika

HomeKitaifa

Ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa yazaa matunda, wafanyabiashara wanufaika

Thamani ya biashara kati ya Tanzania na Ufaransa imekua kwa asilimia 40.6 kwa mwaka 2022 kutokana na kuimarishwa kwa uhusiano baina ya mataifa hayo kulikoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkakati wake wa kuifunga zaidi nchi.

Mwaka 2022 thamani ya biashara kati ya nchi hizi ilifikia TZS bilioni 563 kutoka TZS bilioni 400 iliyorekodiwa mwaka 2021. Kwa upande wa Tanzania mauzo yake kwenda Ufaransa yameongezeka kwa asilimia 116 kufikia TZS bilioni 95 mwaka 2022 kutoka TZS bilioni 44 mwaka 2021.

Mafanikio haya ni matokeo ya mkakati wa Rais Samia kuimarisha diplomasia ya uchumi na kukuza biashara na uwekezaji kupitia ziara yake aliyoifanya nchini Ufaransa Februari 2022 ambapo alipata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo na jumuiya ya wafanyabiashara wa nchi hiyo na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kujionea fursa mbalimbali za kiuchumi.

Baada ya ziara hiyo, Mei 2022 Ujumbe wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi kutoka Ufaransa (MEDEF) ukijumuisha kampuni kubwa 60 kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Peugeot, Thales, TOTAL na Bouygues Construction ulifika nchini kuangalia fursa za uwekezaji kufuatia mwaliko waliopewa na Rais Samia.

Ukuaji wa biashara baina ya mataifa haya unafungua fursa za ajira kwa wananchi katika sekta ambazo bidhaa zake zinasafirishwa kwenda Ufaransa, inaongeza mapato ya Serikali kupitia kodi pamoja na kuongeza fedha za kigeni.

Aidha, Ufaransa na Tanzania zimesaini makubaliano ambayo yataleta matokeo chanya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na makubaliano ya ujenzi wa barabara za mwendokasi, kuimarisha sekta ya kilimo, uchumi wa buluu na usalama baharini.

error: Content is protected !!