Mwindaji wa mamba alifuata sheria

HomeKitaifa

Mwindaji wa mamba alifuata sheria

Uchuguzi unaonesha mwindaji raia wa Marekani, Josh Bowmer katika tukio la kuuwa mamba eneo la kitalu cha Lake Rukwa GR alifuata sheria kwa kuwa na kibali halali, ada na tozo zote za uwindaji alilipa na hakuna utaratibu uliokiukwa.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imetoa taarifa hiyo baada ya kukamilisha uchunguzi wake kuona kama kuna ukiukwaji wa sheria za uwindaji baada ya hivi karibuni kuonekana video mwindaji huyo akifurahia kuwinda mamba mkubwa na kuleta taharuki.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo Januari 02, 2024, TAWA imesema kwa mujibu wa wa taratibu za mkataba wa kimataifa wa CITES, Tanzania imeruhusiwa kuwinda mamba wasiozidi 1,600 kwa mwaka na mpaka sasa jumla ya mamba 39 kati ya 1,600 wamewindwa kwenye mgawo wa taifa wa mwaka 2023.

“Mamba huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita 493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaohitajika kwa mujibu wa sheria, aidha kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Marekani (Safari Club International- SCI), mamba mrefu zaidi duniani aliwindwa chini Ethiopia mwaka 2005 (futi 18.7 sawa na sentimita 561),”

“Vilevile, kumbukumbu zinaonesha, uwindaji huu ulisimamiwa na Askari kutoka TAWA na Mwindaji bingwa kutoka kwenye kampuni iliyopewa kibali kwa mujibu wa sheria, ada na tozo zote zinazohusiana na uwindaji wa mamba zililipwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia uwindaji hapa nchini, hivyo taratibu zote hizi za kisheria zilizingatiwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.” Imeeleza taarifa hiyo.

Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amewahakikishia wananchi kuwa uwindaji wa wanyamapori nchini unazingatia sheria na taratibu za ndani ya nchi na zile za kimataifa hata hivyo mamlaka imewatoa hofu kuwa taratibu hizo zinasimamiwa ipasavyo na ikitokea ukiukwaji hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sharia.

error: Content is protected !!