Jeshi la Polisi mkoa wa Dar es Salaam linamshikilia mfanyabiashara Emmanuel John (38) kwa tuhuma za kutapeli viongozi wa Serikali, wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa kujitambulisha kuwa yeye ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na wengine wawili wakijifanya maofisa wa Serikali na kutapeli viongozi,
Alisema polisi mkoani Geita walianza kuwafuatilia baada ya kufanya mawasiliano na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya na walipofuatilia mawasiliano yao walibaini wahusika wako jijini Dar es Salaam na kushirikiano na polisi wa jiji hilo waliwakamata.
Katika upekuzi watuhumiwa walikutwa na simu na laini nyingi zikiwa na majina ya viongozi wakubwa waandamizi wa Serikali.
Kamanda Mwaibambe alisema Emmanuel amekuwa akipiga simu kwa viongozi akiwapa sifa kuonyesha Rais anaridhishwa na utendaji kazi wao huku akiwataka waendelee kuwa karibu naye kwa kuwa yuko ofisi ya Rais.