Kutokana na mjadala mpana unaondelea kuhusiana na kodi ya pango ya asilimia 10 inayopaswa kulipwa na wapangaji wa nyumba binafsi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi wa suala hilo.
Ufafanuzi huo umeeleza kuwa kodi hiyo si mpya bali ni marekebisho ya kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ambapo wapangishaji wa nyumba binafsi nao wamejumuishwa katika wigo wa kodi tangu Julai mosi mwaka huu.
“Mwenye nyumba atapata cheti cha kodi ya zuio kama ushahidi wa malipo ya kodi iliyolipwa kutokana na zuio la asilimia 10,” inasomeka sehemu ya taarifa ya TRA iliyotolewa jana Agosti 26, 2022.
Kwa ufafanuzi huo wa TRA, wenye nyumba ndiyo watahusika kulipa asilimia 10 ya kodi ya pango kisha watajumuisha fedha hiyo kwenye gharama ya upangishaji wa jengo husika ambapo cheti cha zuio ndicho kitathibitisha iwapo kodi imelipwa.
Kodi ya pango hulipwa kama kodi ya zuio inayotokana na mapato ya pango la nyumba.
Awali Eugenia Mkumbo, Mkuu wa Huduma na Elimu kutoka TRA aliyekuwa katika mafunzo ya wafanyabiashara juu ya mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya mwaka 2022 juzi Agosti 25, 2022 wilayani Bariadi mkoani Simiyu alisema wapangaji ndiyo watakaotoa fedha hiyo ili kurahisisha ukusanywaji.
“Kifungu cha 82 (2) (a) cha Sheria ya Kodi kimefuta msamaha wa kodi kwa wapangaji binafsi hivyo kuwapa mamlaka wapangaji wote kuzuia kodi ya pango katika nyumba binafsi na zile za biashara,” alinukuliwa Mkumbo na vyombo vya habari.
Kodi ya zuio ni nini?
Kwa mujibu wa TRA, kodi ya zuio ni kiasi cha kodi kinachozuiwa na mtu anapomlipa mtu mwingine kutokana na bidhaa zilizosambazwa au huduma iliyotolewa na mlipwaji.
Mtu anayepokea au anayestahili kupokea malipo ambayo kwayo kodi ya mapato inatakiwa kuzuiwa ni mkatwaji wa kodi ilihali mtu anayepaswa kuzuia kodi ya mapato kutoka katika malipo yaliyofanyika kwa mkatwaji anajulikana kama wakala wa kodi ya zuio.
Kifungu hicho cha sheria ni sehemu ya baadhi ya mabadiliko yaliyofanyika katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 iliyoanza kutumika rasmi katika mwaka mpya wa fedha yaani Julai Mosi 2022 baada ya kupitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.