Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametimiza ndoto ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kujenga upya bwawa ambalo litatumika kunyweshea mifugo, wanyamapori na matumizi ya kibinadamu.
Mwalimu Nyerere alijenga bwawa hilo mwaka 1975 kabla ya kupasuka mwaka 1978.
Ulega alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, kukagua bwawa la Kaiwang katika Kijiji cha Ndedo ambalo likikamilika maji yake yatatumiwa na mifugo, wanyama wa porini na binadamu.
Alisema ni fahari kubwa kwa Rais Dk. Samia kutimiza ndoto ya Hayati Mwalimu Nyerere baada ya kufuata maono yake kwa kuhakikisha bwawa hilo linaanza upya kufanya kazi baada ya kujengwa.
Alieleza tayari mkandarasi amefanya utafiti mbalimbali hivyo muda wowote ataanza ujenzi.