Halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe ni miongoni mwa halmashauri zilizopokea fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe, Seuri Mollel ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kufanikisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 250.
“Mwaka jana mwezi wa kumi tulioweza kupata milioni 250 kwa ajili ya kuweza kujenga jengo la ICU, kama unavyojua jiografia ya wilaya yetu ni kilometa 160 mpaka ufike Hospitali ya Mkoa ambapo ndio huduma za dharura zina patikana. Tunaimani kwamba kwa kipindi hiki tunaweza kupata wagonjwa au watu ambao wapo katika hali ya mahututi ambao watahudumiwa hapahapa,” alisema Mollel.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameipatia Wilaya hiyo fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya cha Mundindi ambacho kimepunguza gharama na umbali wa wananchi kufuata huduma ya afya kwenye vituo vya mbali, Mganga Mfawidhi Godfrey Mlwilo anaelezea.
“Watakua wameweza kuokoa gharama ambazo walikuwa wanaweza kusafiri umbali mrefu katika kwenda kufuata huduma kumbe uwepo wa kituo cha afya hapa Mundindi itasaidia watu kupata huduma nyingi ikiwemo huduma za mama na mtoto , upasuaji, huduma za vipimo vya maabara na kadhalika. Kwahiyo kimsingi nafikiri itakuwa ni fursa pia na kwa wananchi jambo lenye furaha,”alisema Mlwilo.