Simu za mkononi zimekuwa ni sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu hasa katika dunia hii ya utandawazi. Wakati mwingine watu hutumia muda mrefu kwenye simu zaidi ya inavyopaswa.
Kuhakikisha kuwa matumizi yako ya simu hayaingiliani na majukumu yako mengine fanya haya;
Weka muda unaopaswa kutumia simu yako na kufanya nini ili kuepuka kushika simu mara kwa mara na kupoteza muda wa kufanya mambo mngine. Unaweza kusema asubuhi nitatumia dakika 30 kusoma na kujibu meseji kila asubuhi saa 7:00 -7:30 na jioni, saa 16:00 jioni nitapekua mitandao ya kijamii kwa dakika 30 na kuendelea kupanga bila kusahau kujiachia muda wa wewe kupumzika na kufanya mambo ambayo hayahusishi kuwa na simu mkononi.
Kitanda sio meza ya simu. weka simu yako mbli na kitanda hata kama unaitumia kwa ‘alarm’. Kupanda kitandani na simu kunapelekea kucheza na simu muda ambao ulipaswa kulala na hivyo kukosa usingizi wa kutosha kiafya.
Panga kuonana na watu uso kwa uso kuliko kutegemea kumaliza maongezi kwa njia ya simu. Iwe ni kumpa taarifa fulani, makutano ya kibiashara ama kustarehe. Hii itasaidia kukuza mahusiano yako na watu hao.
Jichanganye na watu. Badala ya kutumia saa 4 kucheza video mtandaoni, jaribu kujiunga kwenye kikundi cha michezo, itakusaidia kujifunza mambo kadhaa kutoka kwa wengine na kukupa uzoefu utakaoweza kutumia hapo baadaye.