Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema linawasaka watuhumiwa waliohusika katika vurugu za kuwatorosha watuhumiwa waliokuwa wamekamatwa, tukio lililosababisha kifo cha mtu mmoja.
Tukio hilo limetokea leo, Novemba 5, 2026, majira ya saa 12:00 asubuhi katika Kitongoji cha Msungwe, Kata ya Kapele, Wilaya ya Momba
Taarifa iliyotolewa na polisi imesema awali, askari Polisi walifika katika eneo hilo kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la shambulio la kudhuru mwili lililotokea Novemba 4, 2026. Katika tukio hilo, vijana wawili walishambuliwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mili yao baada ya kuvamiwa wakiwa katika shamba walikokuwa wakifanya kazi.
“Baada ya kufika katika eneo hilo, askari walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili na kuanza safari ya kuelekea mahali walipokuwa wameegesha gari. Hata hivyo walipokuwa karibu na eneo hilo, walisikia mayowe na kuzingirwa na kundi linalodaiwa kuwa la wafugaji, ambao walianza kuwashambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi,” imeeleza taarifa ya polisi.
Imeongeza kuwa, “kutokana na hali hiyo, askari walilazimika kujihami kwa kufyatua mabomu na risasi hewani na kufanikiwa kulitawanya kundi hilo. Katika vurugu hizo, watuhumiwa waliokuwa wamekamatwa walifanikiwa kutoroka pamoja na kundi hilo wakiwa na pingu mikononi.”
Polisi wamesema baada ya vurugu hizo zilizoanzishwa na kundi hilo kwa lengo la kuwatorosha watuhumiwa, ilibainika kuna mtu mmoja amejeruhiwa, na baada ya kufikishwa hospitalini mtu huyo tayari alikuwa amefariki.


