Rais atatimiza ahadi yake Mei Mosi?

HomeKitaifa

Rais atatimiza ahadi yake Mei Mosi?

Macho na masikio ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi yataelekezwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi sherehe za Mei Mosi mwaka huu huku baadhi ya wafanyakazi wakiwa na matumaini makubwa ya kupata nyongeza ya mishahara.

Hiyo itakuwa mara ya pili kwa Rais Samia kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka 2021 akichukua nafasi ya Hayati John Magufuli.

Macho na masikio ya wafanyakazi yatakuwa kwake ili kufahamu atazungumza nini kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao hasa kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma na ile ya sekta binafsi na kupandisha madaraja wafanyakazi wa umma.

Jambo lingine ambalo litaibua mjadala katika sherehe hizo ambazo zinazofanyika kila mwaka ni nyongeza ya mishara kwa watumishi wa umma na kupungua kwa kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) ambacho kwa sasa ni asilimia nane kilichoanza kutumika mwaka jana.

Swali linabaki, Rais atatimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka jana katika sherehe za Mei Mosi za mwaka jana zilizofanyika kitaifa mkoani Mwanza?

Rais Samia alisema hawezi kuongeza mishahara ya wafanyakazi hadi mwaka huu wa 2022 kutokana na kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za uchumi na janga la Corona (Uviko-19).

Pia alisema alishindwa kuongeza mishahara kutokana na hatua anazopanga kuchukua za kufuta kodi na tozo zilizokuwa zinawabughudhi Watanzania zilizosababisha kupungua kwa mapato yatokanayo na kodi.

“Lakini niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa mwakani siku kama ya leo (Mei Mosi 2022) nitakuja na package (kifurushi) nzuri ya kupandisha mishahara,” amesema Rais Samia katika hutuba yake ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na watu wengi hasa wafanyakazi.

Kwa miaka zaidi ya sita sasa watumishi wa umma na sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia kutopandishiwa mishahara na kuwa na maslahi duni licha ya gharama za maisha kupanda kila siku.

Huenda wakafutwa machozi katika sherehe za mwaka huu, kama walivyo na matarajio makubwa ya kuboresha maisha yao.

SOURCE: NUKTA HABARI

error: Content is protected !!