Wakati anamalizia ziara yake Arusha leo katika uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Elias Food Overseas Ltd na uzinduzi wa mradi wa maji Longido, Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpaka kufikia Desemba mwaka 2022 vijiji vyote 133 ambavyo havijafikiwa na umeme vitapata umeme na Arusha yote itawaka umeme kwa asilimia 100.
Samabamba na ahadi ambayo Rais Samia ameitoa pia amaeelezea umuhimu wa kuzinduliwa kwa mradi huo wa maji uliogharimu pesa za Kitanzania shilingi bilioni 15.7 utachochea mafanikio makubwa Longido kwani kuwepo kwa maji safi na salama kutapelekea kuongezeka kwa wawekezaji na shughuli za kiuchumi.
Longido imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu kutokana na jiografia ya eneo hilo, lakini leo mradi huo wa maji uliozinduliwa na Rais alionja maji hayo kama ishara ya kuwathibitishia wana Longido maji ni safi na hayana chumvi.
Pamoja na kuwepo kwa miradi mingi ambayo serikali inaendelea kuzindua pia Rais amesema wanatambua tatizo la ajira kwa vijana na kama serikali kitaifa wameanza kutafuta suluhisho la changamoto ya ajira kwa kuanzisha mitaa ya viwanda kila mkoa ili kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania.