Rais Samia atoa maagizo jinsi yakupunguza ajali za barabarani

HomeKitaifa

Rais Samia atoa maagizo jinsi yakupunguza ajali za barabarani

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua wiki ya nenda kwa usalama barabarani huku akiagiza elimu ya matumizi sahihi ya barabara ielekezwe zaidi kwa madereva wa bodaboda ili kujikinga na ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa Rais Samia, asilimia 90 ya ajali za barabarani husababishwa na binadamu huku kundi linaloathirika zaidi ni vijana wanaoendesha bodaboda ambapo vijana 400 hufariki dunia kwa ajali za barabarani kila mwaka huku wengine zaidi ya 800 hulazwa katika hospitali kutokana na kujeruhiwa. 

Amesema pia asilimia 3.2 ya ajali hizo husababishwa na ubovu wa barabara na asilimia 1.3 husababishwa na utelezi.

“Bado waendesha bodaboda ndiyo chanzo cha ajali hizi, niombe wakati baraza la usalama barabarani likiwa linatoa elimu libaki na kundi hili kwa kuwa ndiyo waathirika wakubwa,  bado hawazingatii sheria,  hawavai kofia ngumu na uendeshaji usiozingatia sheria, ” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata sheria bila shurutu na kuwa mlinzi kwa mwenzake ili kuweza kudhibiti ajali huku akiagiza kufanyika kwa  utafiti wa kimfumo kwa kushirikiana na wadau  mbalimbali wa usalama barabarani na vyuo  ili kuja na mipango ya kupunguza ajali hizo huku polisi wakitakiwa kuwa msaada na rafiki kwa wananchi.

“Na hapa naomba nisistize zipo tabia za baadhi ya askari wa usalama barabarani kushikilia leseni za madereva,  madereva kulazimishwa kulipa deni alilokamatwa nalo papo hapo,  pamoja na ukamataji wa vyombo vyao kwa muda mrefu,  suala hili liangaliwe upya ili kupunguza hizo kero ndogo ndogo,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!