Serikali yatamba kushamiri kwa Demokrasia nchini ndani ya miaka 60 ya Uhuru

HomeKitaifa

Serikali yatamba kushamiri kwa Demokrasia nchini ndani ya miaka 60 ya Uhuru

Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, kumekuwa na maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi nchini sambamba na udumishwaji wa amani, utulivu, uzalendo na umoja wa kitaifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, na Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema hayo jana jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Ofisi ya Waziri Mkuu tangu Tanzania bara kupata Uhuru mwaka 1961.

Alisema mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ulikuwapo nchini kabla ya uhuru na mara baada ya uhuru. Jenista alisema kati ya mwaka 1965 mpaka 1992 kulikuwa na mfumo wa chama kimoja na mwaka 1992 nchi ilirejesha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ili kupanua wigo wa demokrasia.

Alisema mwaka 1992 Sheria ya vyama vya siasa namba 5 ilitungwa na kuanzishwa kwa ofisi ya usajili wa Vyama vya Siasa nchini na kwamba vyama vya siasa vilianza kusajiliwa tena mwaka huo wa 1992.

Alisema pia katika uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1992, vyama 13 vilivyopata usajili vilishiriki katika uchaguzi huo, na tangu mwaka huo hadi hivi sasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeshatoa vyeti vya usajili wa muda kwa vyama vya siasa 81 na imetoa vyeti vya usajili kamili kwa vyama vya siasa 25 na kufuta usajili wa vyama vya siasa vyenye usajili kamili sita ambavyo vilikiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.

Tangu sheria ya vyama vya siasa kutungwa, sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mara nane mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2019.

Serikali imesema kuwa marekebisho ya ya mwaka 2009 Sheria ya Vyama vya Siasa ilianzisha Baraza la Vyama vya Siasa ambalo ni chombo kinachokutanisha vingozi wa kitaifa vya vyama vya siasa vyenye usajili kamili kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi nchini sambamba na kudumisha amani, utulivu, uzalendo, umoja wa Taifa.

Pia Waziri Jenista alisema kumekuwa na mageuzi makubwa katika uendeshaji uchaguzi Mkuuu kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuboresha mifumo iliyoongeza tija ya utendaji kazi.

error: Content is protected !!