Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo kuchimba mchanga kwa sababu vitendo hivyo vinasababisha hasara kwa Serikali.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza jijini Arusha Julai 22, 2022 wakati wa ufunguzi wa barabara ya Afrika Mashariki (Arusha Bypass) yenye urefu wa kilomita 42.4 amesema kila mwananchi anawajibika kutunza miundombinu ya barabara ili iwanufaishe katika shughuli za usafirishaji.
“Niwaombe sana ndugu zangu kufuata taratibu zilizowekwa ili tuendelee kutunza miundombinu yetu, iendelee kutukuzia uchumi wetu,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi na kueleza kuwa,
“Kumeanza kujitokeza vitendo viovu vya kuharibu miundombinu yetu. Kila siku tunaona Jeshi la Polisi wakizungumzia jinsi ya kutunza barabara zetu kutokutengeneza magari yanayoharibika barabarani kwa sababu wanapofanya hivyo wanamwaga mafuta ambayo yanakwenda kutoboa barabara zetu.”
Lakini suala la kuzidisha uzito wa magari yetu na lenyewe linakwenda kuharibu barabara zetu
Amesema vitendo vingine vinavyoharibu miundombinu ni kuzidisha uzito wa mizigo kwenye magari, kutupa taka kwenye madaraja na kuchimba mchanga.
Aidha, Rais Samia amesema barabara hiyo ya Afrika Mashariki itakuwa kiungo muhimu cha shughuli za biashara na utalii kati ya Kenya na Tanzania.
Barabara ya kimataifa ya Arusha-Holili hadi Taveta, Voi nchini Kenya, awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Sakina- Tengeru yenye urefu wa Kilomita 14.1 iliyojengwa kwa njia mbili kila upande, na barabara ya mchipuo ya jiji la Arusha yenye urefu wa kilomita 42.4.
Akizungumza katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo, Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema barabara hiyo itakuwa na manufaa mengi ikiwemo kuongeza ukaribu wa wananchi, kuimarisha biashara na kurahisisha usafirishaji wa mizigo na bidhaa katika nchi hizo.
“Huo ni utajiri kwa wakulima wa Tanzania na wafanyabiashara wa Kenya na njia ya kumaliza umasikini katika nchi zetu,” amesema Rais Kenyatta huku akieleza kuwa miundombinu ndiyo msingi wa maendeleo.