Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika kumuenzi baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya ujinga, maradhi pamoja na njaa.
Msimamo huo wa Serikali umekuja siku moja kabla ya kuadhinisha kifo cha Mwalimu Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999.
Rais Samia amewaambia Watanzania waliohudhuria hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa Chuo Cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera leo Oktoba 13, 2022 kuwa hata baada ya Mwalimu Nyerere kukabidhi madaraka Serikali zilizofuata zimeendeleza mapambano dhidi ya maadui hao watatu.
“Miaka 23 bila Mwalimu Nyerere, bado Serikali zetu zinaendelea kupiga vita maadui hawa na vita hii itaendelea kuwepo kwa sababu idadi ya watu inaongezeka na kila wanaozaliwa wana mahitaji hawa,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema licha ya Serikali kufanya kazi kubwa ya kuondoa ujinga bado vijana wengi hawana ujuzi na stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa hivyo chuo hicho kitakuwa na kazi ya kuongeza thamani kwenye ujuzi uliotolewa awali.
Katika kutengeneza mazingira ya vijana kujiajiri mara watapohitimu katika chuo hicho Rais Samia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamira, wakuu wa wilaya na halmashauri kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya fedha za halmashauri ili ziwasaidie vijana kujiajiri.
“Vijana hawa watakaoingia hapa wajulikane mna asilimia 10 za halmashauri, wanapohitimu wakute pesa halmashauri ipo tayari aidha kuwapa pesa au kuwanunulia vifaa ambayo ni nzuri Zaidi,” amesema Rais.
Itakumbukwa kuwa Tanzania imekuwa inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la ukosefu wa ajira kutokana na watu kukosa ujuzi unaohitajika au kukosa fedha za mitaji hivyo chuo hicho kinatarajiwa kitapunguza wimbi hilo.
Chuo hicho cha Veta kilichojengwa Burugo mkoani Kagera kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,500 ambapo ujenzi wake pamoja na vifaa vya kufundishia ikiwemo mashine na karakana vimefadhiliwa na Serikali ya China.