Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amempongeza na kumshukuru Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume ya maboresho ya mifumo ya taasisi za haki jinai Tanzania ili kuleta tija kiutendaji kwa mifumo ya hiyo kwa mahitaji ya sasa.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Aprili 11, 2023 alipokutana na tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande.
Aidha, Dk.Mwinyi amesema ana matarajio makubwa ya mapendekezo kupitia ripoti ya tume hiyo ambayo itawasilishwa kwa Rais Dk Samia nakuonyesha marekebisho yanayohitajika katika mfumo mzima wa kimuundo wa taasisi za haki jinai kwa kuleta ufanisi mkubwa wa utekelezaji wa utoaji haki kiufanisi zaidi na manufaa kwa serikali zote mbili.
Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema tume hiyo itazungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, asasi za kiraia na kiserikali , pamoja na taasisi zinazoshughulikia haki jinai Jeshi la Polisi, Chuo cha Mafunzo , Mamlaka ya kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar, Uhamiaji , Mahakama n.k. Pia watazuru Mikoa ya Unguja na Pemba kwa siku nne kukutana na makundi hayo.
Tume hii iliteuliwa na kuzinduliwa na Rais Dk Samia Januari 30, 2023 kutathmini na kuangalia maboresho ya mifumo ya haki Jinai Tanzania.