Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito wa kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto ya mfumo wa kimataifa wa kifedha, unaozuia upatikanaji wa fedha za muda mrefu na za gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo katika nchi zinazoendelea.
Rais Samia ametaka iwepo jitihada maradufu na matokeo ya namna ya kushughulikia tofauti za kaskazini-kusini mwa Dunia ili kuwa na mkakati thabiti wa kifedha, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi ulio na msingi wa uchumi wa kimataifa.
Akizungumza katika kilele cha majadiliano ya mkutano wa 15 wa Wakuu wa nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICS) uliofanyika jana Jijini Johannesburg, Rais Samia amesema kwa sasa Dunia inakabiliwa na changamoto nyingi.
“Jumuiya ya Kimataifa lazima iwe moja na iwe tayari kupambana na masuala kama umaskini, tabiachi na upungufu wa chakula,” amesema Rais Samia.