Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi bwawa kubwa la umwagiliaji linalohusishwa na kiwanda cha sukari cha Mtibwa, ambalo linatajwa kuwa bwawa kubwa zaidi katika Afrika Mashariki na Kati. Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa uwekezaji huo na jinsi ulivyosaidia kukuza uzalishaji wa sukari nchini.
“Uwekezaji huu uliozidi umewezesha kukuza uzalishaji wa sukari kutoka tani 15,000 mwaka 2007 hadi tani 82,500 zinazotarajiwa mwaka huu,” alisema Rais Samia, akionyesha hatua kubwa iliyopigwa na sekta ya sukari katika kipindi cha miaka michache iliyopita.
Rais Samia pia alieleza kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu, hatua inayolenga kufungua masoko mapya kwa bidhaa za Tanzania. “Tunajenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu ili tufikie masoko makubwa,” aliongeza Rais Samia.
Akiangazia masoko ya kikanda, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania inalenga kuingia kwenye soko la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), soko ambalo alilitaja kuwa kubwa mno. “Tunalenga kufika DRC, DRC ni soko kubwa mno kwahiyo sukari yote itakayozalishwa Tanzania italiwa ndani lakini tutaweza kuuza kupita Burundi, DRC na nchi zitakazotaka sukari yetu hatutakuwa na shida ya usafiri,” alisisitiza.
Katika kuunga mkono sekta ya sukari, Rais Samia alifichua kuwa serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kwa viwanda vya sukari nchini, huku ikitoa mfano wa kiwanda cha Mtibwa ambacho kimesamehewa kodi yenye thamani ya shilingi bilioni 80.9 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. “Serikali imekuwa ikiunga mkono sekta ya sukari ikiwemo kutoa misamaha ya kodi, kodi inayosamehewa na serikali kwa viwanda vya sukari 5 nchini ni shilingi bilioni 246.660,” alisema Rais Samia.
Akitazama mbele, Rais Samia aliwahimiza wawekezaji na wadau wa sekta ya sukari kuendelea na juhudi zao za kuongeza uzalishaji, akilenga kufikia uzalishaji wa tani 150,000 ifikapo mwaka 2028/29. “Nataka niwatie moyo kuendelea kutekeleza Dira ambayo mmejiwekea inayoelekea kwenye uzalishaji wa tani 150,000 ifikapo mwaka 2028/29,” alisema.
Rais Samia alihitimisha kwa kusisitiza jukumu la serikali katika kulinda na kutetea maslahi ya makundi yote katika jamii, akibainisha kuwa serikali inasimamia haki za makundi yasiyo na nguvu ili kuhakikisha usawa na ustawi kwa wote. “Jukumu la serikali ni kulinda na kutetea maslahi ya makundi yote katika jamii, hivyo inapotokea serikali inasimamia upande wa kundi lisilo na nguvu ni katika kutimiza jukumu hilo na kutetea maslahi ya makundi yote katika jamii,” alihitimisha Rais Samia.