Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali inajipanga kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na janga la UVIKO-19 duniani pamoja na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukreini.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa kusaidia uchumi ni kuhakikisha kunakuwa na ardhi, nguvu kazi, mtaji na kuongeza wanawake katika nafasi za maamuzi.
Rais Samia ameyamesema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika kongamano la siku ya wanawake lililofanyika Zanzibar.
Pamoja na hayo amesema uchumi wa dunia umeyumba hivyo mataifa makubwa yamepunguza kusaidia nchi za mataifa yanayoendelea badala yake wanataka kufanya biashara hususani za mboga mboga, matunda na chakula.
Aidha uwepo wa biashara hizo ni fursa kwa wanawake kutumia fursa hiyo kufanya kazi.Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa upande wa Tanzania yamefanyika katika kila mkoa lakini pia yamefanyika Zanzibar.
Kauli mbiu za maadhimisho haya kwa mwaka huu, kwa Upande wa Zanzibar ni “zingatia usawa wa kijinsia ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa maisha endelevu Zanzibar” na kitaifa kauli mbiu ni “kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu jitokeze kuhesabiwa”.