Rais Samia: Niwaombe sana kachanjeni

HomeKitaifa

Rais Samia: Niwaombe sana kachanjeni

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwataka Watanzania kujikinga dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kufuata taratibu zote za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19

Rais Samia amesema hayo jana kwenye mkutano wake wa hadhara na wananchi wa Mkoa wa Iringa uliofanyika katika uwanja wa Samora.

“Niungane na Mheshimiwa Waziri wa Afya Dada Ummy kuhusu kinga dhidi ya UVIKO-19, tunavyotembea hivi bila kuvaa viziba pua na mdomo tunajidanganya kwamba maradhi yamekwisha” amesema Rais Samia

Rais Samia amewataka wananchi kuendelea kujikinga dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19.

“Kinga ya ugonjwa huu ni kwenda kuchanja, niwaombe sana wananchi wote kachanjeni” amehimiza Rais Samia Suluhu Hassan

Awali akizungumza, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa huo bado upo nchini na unaendelea kuleta madhara makubwa kwa watu ambao hawajachanja chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

“Nikiangalia takwimu, Mwezi Juni tulikuwa na wagonjwa 352, Mwezi Julai wagonjwa wameongezeka mpaka 543” amesema Waziri Ummy akiwa anataja Takwimu za ugonjwa huo.

Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa za kitaalam, tunaweza kuishi na UVIKO-19 endapo tutajenga kinga kwa jamii ambayo inatulazimu kuchanja angalau asilimia 70 ya Watanzania.

“Ninawahimiza sana wana Iringa kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili tuweze kuishi na ugonjwa huu kama tunavyoishi na mafua ya kawaida” amesisitiza Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema chanjo ina umuhimu kwa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 huku akisema kwa tafiti aliyoifanya kwa wagonjwa 10 waliolazwa kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 wote walikuwa hawajapata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

error: Content is protected !!