Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Shahada ya Heshima (Honorary Doctorate) wakati wa ziara yake ya kiserikali nchini Urusi.
Tuzo hiyo ilitolewa na Mkuu wa Chuo Kikuu (Rector), Profesa Oleg Yastrebov, kwa kutambua mchango wa Rais Samia katika mageuzi ya sekta ya elimu, juhudi zake za kuimarisha diplomasia ya Tanzania, pamoja na nafasi yake katika kuitangaza Tanzania kimataifa, ikiwemo kupitia sekta ya utalii.
Heshima hiyo imetolewa katika kipindi cha ziara rasmi ya kiserikali ya Rais Samia nchini Urusi, iliyoanza Juni 2 kufuatia mwaliko wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Katika ziara hiyo, Rais Samia pia aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo ya pande mbili na Rais Putin pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali ya Urusi yaliyofanyika katika Ikulu ya Kremlin. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria kati ya Tanzania na Urusi.
Kwa mujibu wa maafisa wa Tanzania, ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati na kupanua ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza Ajenda ya Maendeleo ya Dira ya Taifa ya 2050.
Rais Samia aliwasili jijini Moscow kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo, katika ziara ya kihistoria inayolenga kuendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali.




