Rasmi DP World kuendesha sehemu ya bandari ya Dar kwa miaka 30

HomeKitaifa

Rasmi DP World kuendesha sehemu ya bandari ya Dar kwa miaka 30

Tanzania imesaini mikataba mitatu na kampuni ya DP World ya Dubai ya kukodi na kuendesha sehemu ya bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 30, miezi minne baada ya kuwepo upinzani mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uwekezaji huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa amesema mikataba iliyosainiwa inajumuisha mkataba wa nchi mwenyeji (Host Government Agreement) na mikataba miwili ya ukodishaji na uendeshaji wa bandari kubwa zaidi nchini.

Pamoja na kuingia mikataba hiyo kwa miaka 30, Mbossa amesema utendaji wa DP World utakuwa ukipimwa kwa kila miaka mitano kuhakikisha viwango walivyokubaliana vinataekelezwa ipasavyo.

“Pia, Serikali kupitia TPA itakuwa na umiliki wa hisa katika kampuni itakayokuwa ikifanya kazi katika bandari ya Dar es Salaam…jukumu la ulinzi wa maeneo ya bandari litabaki chini ya Serikali na sheria za Tanzania zitatumika katika utekelezaji wa mikataba hii,” amesema.

Katika mikataba hiyo, miongoni mwa makubaliano ni kuwapa uhuru wafanyakazi wa sasa wa TPA kuhamia DP World ama kubaki katika shirika hilo la umma.

Kutiwa saini mikataba hiyo, kwa mujibu wa Mbossa, kutasaidia kuongeza ufanisi katika bandari hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ucheleweshaji katika uondoshaji wa mizigo na meli kukaa muda mrefu nangani kwa zaidi ya siku tano.

TPA yasaka wawekezaji gati 8 hadi 11

Mbossa amesema DP World amekodishwa na kupewa kandarasi ya kuendesha gati namba nne hadi saba la bandari ya Dar es Salaam na kwamba Serikali kwa sasa inatafuta wawekezaji wengine kuwekeza gati namba nane hadi 11.

Katika mikataba hiyo, Mbossa amesema Serikali itakuwa inabaki na asilimia 60 ya mapato yote kutokana na gharama zote za uendeshaji kubakia kwa DP World. Hapo awali, amesema Serikali ilikuwa inatumia takribani asilimia 90 ya mapato yaliyokusanywa katika uendeshaji wa maeneo hayo yaliyokodishwa na kubakiwa na asilimia 10 tu ya mapato yote

Hatua ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma leo (Oktoba 22, 2023) inakamilisha safari ya majadiliano ya kiuwekezaji baina ya Serikali na kampuni hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Dubai ambayo yaligubikwa na upinzani mkubwa kutoka kwa umma kuanzia mapema Juni mwaka huu.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa DP World Sultan Ahmed Bin Suleym amesema kuingiwa kwa mikataba hiyo ni hatua muhimu kwa kampuni hiyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania ikiwemo kuifanya kuwa kitovu cha masuala ya uchukuzi Afrika.

DP World kuwekeza Sh612.5 bilioni 

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutawekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 250 (Sh612.5 bilioni) kuboresha bandari. Tutawekeza zaidi katika ujenzi wa mifumo ya kuondosha kwa kasi mizigo ili kupunguza ucheleweshaji unaozikumba kampuni za meli kwa sasa,” amesema Suleym.

Bosi huyo wa DP World amesema watajitahidi kuimarisha nafasi ya bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la nchi za ukanda wa shaba na madini mengine muhimu ulimwenguni.

Kwa takriban miezi minne sasa kumekuwa na upinzani mkali juu ya uwekezaji wa DP World katika bandari ya Dar es Salaam kutoka kwa watu na makundi mbalimbali wakiwemo maaskofu wa kanisa katoliki, wanaharakati na wanasiasa wa upinzani baada ya Bunge kuridhia mkataba baina ya Tanzania na Serikali ya Dubai Juni mwaka huu.

Katika hotuba yake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imezingatia maoni ya wadau wote wakati wa majadiliano ya mikataba hiyo.

“Hakuna kundi ama sauti iliyopuuzwa. Tuliunda jopo la wataalamu kusikiliza maoni…baadhi ya waliofanya uchambuzi kutoka sekta binafsi waliingizwa kwenye timu ya majadiliano,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!