Ripoti ya Pili: Mhudumu ndiye aliyefungua mlango

HomeKitaifa

Ripoti ya Pili: Mhudumu ndiye aliyefungua mlango

Mapya yaibuka Ripoti ya Pili ya Taasisi ya Uchunguzi wa Ajali ya Ndege (AAIB) iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhusu ajali ya ndege ya Precision Air iliyoanguka Ziwa Victoria baada ya kushindwa kutua Bukoba, mkoani Kagera.

Ripoti hiyo ambayo ni tofauti na ile ya kwanza, imetegua kitendawili cha nani hasi alifungua mlango wa ndege kati ya wahudumu na mvuvi Majaliwa Jackson, shujaa aliyetambulishwa nchini ikisema ni wahudumu wawili wa Precision Air.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uchunguzi wa Ajali za Ndege, Redemptus Bugumola alisema ripoti hiyo ya pili ina tofauti na ile ya kwanza iliyotoka Novemba 23 mwaka jana.

“Lakini hii ya pili tulikwenda mbali zaidi, kama unavyojua kuna vinasa sauti ambavyo vinakuwa katika ndege. Kuna kimoja kinanasa sauti ya mawasiliano ya rubani na mwenzake au matangazo yaliyokuwa yakitolewa kwa abiria,” alisema Bugumola.

Ripoti hiyo imeeleza kwamba, wakati ndege ikikaribia kutua Bukoba, kulisikia sauti mara tatu ikiwaonya marubani kuwa wako karibu na kugusa ardhi lakini wachunguzi wanasema marubani hawakufanya lolote.

Pia imenukuu sauti za majadiliano ndani ya ndege hiyo na rubani msaidizi alisikika akipaza sauti mara mbili tofauti akimtaka rubani mkuu kuacha kutua na airushe ndege juu lakini hakujibiwa.

Mbali na hilo, ripoti inaeleza kuwa waongozaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza waliwajulisha marubani na kuwashauri kwenda kutua Mwanza lakini wao waliamua kutua Bukoba.

NANI ALIFUNGUA MLANGO?

Ripoti hiyo imeeleza mhudumu mmoja ndiye aliyefungua mlango wa abiria kwa kusaidiwa na abiria aliyekuwa na nguvu ambao abiria wengi walitokea na mhudumu mwingine alifungua mlango wa dharura na kutumbukia majini.

Aidha, wavuvi waliokuwa jirani, ripoti inaeleza walifika eneo hilo dakika tano baada ya ajali kutokea na ndio waliowahamishia kwenye mitumbwi abiria 24 na wahudumu wawili walionusurikia kati ya watu 43 waliokuwemo kwenye ndege.

Kutokana na maelezo ya ripoti hiyo, ushujaa wa Majaliwa unaotambulika ndani na nje ya Tanzania umepotea kwani hakuna sehemu inayoeleza kwamba ndiye aliyefungua mlango kama ambavyo alieeleza.

Ripoti hiyo inasema abiria 19 waliokaa viti vya mbele na katikati hawakuweza kujiokoa baada ya ndege kuanguka, walifunikwa na maji na kuzama hivyo kupoteza maisha.

 

 

error: Content is protected !!