Ruksa kuwekeza Msomera

HomeKitaifa

Ruksa kuwekeza Msomera

Serikali imefungua milango ya fursa za uwekezaji katika kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ili kuboresha maisha ya wakazi wa Ngorongoro waliohamia katika kijiji hicho.

Zoezi la kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro katika kijiji cha Msomera lilianza Juni 2022 lengo likiwa ni kulinda ekolojia ya hifadhi hiyo ya Taifa itayotajwa kuwa miongoni wa vivutio vya utalii vikubwa Afrika Mashariki.

Ili kutekeleza zoezi hilo Serikali ilitenga Sh700 bilioni iliyowezesha ujenzi wa nyumba za vyumba vitano kila moja, kuwalipa wakazi hao fidia na kujenga miundombinu mingine itakayowawezesha kuishi katika kijiji hicho.

Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi aliyekuwa akizungumza katika mkutano na wanahabari uliofanyika jijini Tanga, Januari 17, 2023 amesema baada ya awamu kadhaa za kuhamisha wakazi hao hivi sasa Msomera ipo wazi kwa uwekezajii.

“Hakuna ugumu wowote wa muwekezaji kufika katika eneo lolote la nchi yetu ilimradi anafuata taratibu, wawekezaji wa nje na wa ndani wanaruhusiwa kufika kama ilivyo katika maeneo mengine…

“…Ni wao tu kuchangamka au wananchi wenyewe wa hapa kuchagamka. Serikali inachofanya ni kuweka vivutio ili mwekezaji aweze kufika,” amesema Matinyi.

Msemaji huyo amebainisha kuwa miongoni mwa shughuli za uwekezaji zinazoweza kuanzishwa katika kijiji hicho ni ujenzi wa maduka, sehemu za burudani na viwanja vya michezo ambazo zote zinawezekana kutokana na ukubwa wa eneo hilo.

Kufunguliwa kwa fursa hiyo ya uwekezaji Msomera kunatoa nafasi kwa wakazi wa kijiji hicho waliohamishwa kutoka hifadhi ya Ngorongoro ambayo kisheria haikuruhusu uwekezaji kuishi maisha ya kisasa tofauti na ya wali.

Kwa mujibu wa Matinyi mpaka sasa jumla ya kaya 677 zenye watu 3,822 na mifugo 18,102 zimehama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia katika kijiji cha Msomera.

Idadi hiyo ya kaya zilizohamia Msomera ni sawa na asilimia 0.3 ya lengo la Serikali la kuhamisha kaya 22,000 zilizopo Ngorongoro.

Ili kuboresha maisha ya wakazi hao, Matinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu mingine katika kijiji hicho ikiwemo ujenzi wa hospitali, madarasa, barabara, mnada, malisho ya mifugo, vituo vya kuuza maziwa pamoja na miundombinu ya mawasiliano.

error: Content is protected !!