Rais wa Kenya, William Ruto, ameikosoa vikali taasisi ya Ford Foundation kwa madai ya kufadhili vurugu nchini humo. Akizungumza mbele ya umma, Ruto aliuliza, “Mimi nataka niulize watu wa Ford Foundation watuambie hiyo pesa wanatoa ifanye fujo ndio wapate faida gani.”
Rais Ruto aliongeza kuwa kama taasisi hiyo itaendelea kufadhili uvunjaji wa amani kupitia maandamano, serikali yake italazimika kuwaambia waache kufadhili au waondoke nchini Kenya. “Kama wanaendelea kufadhili uvunjaji wa amani kupitia maandamano tunaenda kuwaambia wachague kuacha kufadhili au waondoke Kenya,” alisema.
Aidha, Ruto alisisitiza umuhimu wa kuwapa vijana ajira badala ya kuwashawishi kujiingiza kwenye vurugu. “Vijana sio wakufanya fujo, vijana ni wakufanya kazi na huo ndio mpango tupo nao kupanga ajira za hawa vijana,” alieleza.
Maneno ya Rais Ruto yanakuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la maandamano na vurugu nchini Kenya, hali ambayo imezua hofu kuhusu usalama na utulivu wa nchi. Taasisi ya Ford Foundation haijatoa tamko rasmi kuhusu tuhuma hizo za Rais Ruto.