Sababu za serikali kutositisha Mbio za Mwenge

HomeKitaifa

Sababu za serikali kutositisha Mbio za Mwenge

Rais Samia Suluhu Hassan leo ameongoza Watanzania katika kuzima Mwenge wa Uhuru pamoja na maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 22 ya Kifo cha Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana, halfa zilizofanyika kwa pamoja mkoani Geita.

Mbio za Mwenge wa Uhuru ni utaratibu ambao umekuwepo nchini kwa miaka mingi sana, zikitumika kama hamasa ya maendeleo. Licha ya viongozi kuendelea kuona umuhimu wake, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitaka serikali iachane na utaratibu huo kwa madai kuwa unaiingiza nchi kwenye gharama zisizo za msingi.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi anaamua kutumia Tawasifu yake, Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu kueleza chimbuko na umuhimu wa mwenge huo kwa Tanzania na Afrika.

Anaanza kwa kuandika kuwa kwa asili, mbio za Mwenge zilianzishwa na kuendeshwa kama shughuli ya chama cha TANU (baadae Chama cha Mapinduzi), lakini mwaka 1994 chini ya Serikali ya awamu ya pili, mbio za Mwenge ziliondolewa kwenye ratiba za chama na kutambulika kama shughuli rasmi ya Serikali.

Mzee mwinyi ameandika kwamba sababu ya kwanza ya kuwepo kwa mbio za Mwenge inahusiana sana na ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere kwamba, “Sisi [Tanzania] tunataka kuwasha mwenge na  kuuweka juu ya Mlima wa Kilimanjaro ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete upendo pale ambapo kuna chuki, heshima pale ambapo pamejaa dharau, na matumaini pale ambapo hakuna matumaini.”

> Ahadi 6 za Rais Samia kwa wakazi wa Chato

Mzee Mwinyi amesisitiza “Ndiyo maaa ukaitwa Mwenge wa Uhuru- uhuru wa bara la Afrika na uhuru wa Mwafrika. Kwa maneno mengine, hata kabla ya uhuru, dhana ya Mwenge wa Uhuru ilikuwa chanzo na kielelezo cha iliyokuja kuwa sera ya mambo ya nje ya Tanzania huru kuhusu ukoloni na ubaguzi wa rangi barani Arika.”

Baada ya kupatikana kwa uhuru wa mataifa ya Afrika, Mwenge wa Uhuru umeendelea kubaki kuwa alama muhimu ya ukombozi lakini pia ukiendeleza lengo lake la pili kama ilivyoelezwa kwenye ukurasa wa 419 wa Tawasifu ya Mzee Rukhsa.

“Kuzima koleo sio mwisho wa uhunzi, na kuingia madarakani kwa serikali ya weusi walio wengi Afrika Kusini haukuwa mwisho wa mapambano yanayobebwa na dhana ya Mwenge wa Uhuru. Nami nikatumia fursa ile kufafanua kuhusu dhana mpya Mbio za Mwenge ambayo ilikuwa kutoa fursa ya kipekee ya kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo yao kwa njia ya kujitolea. Hivyo wakati wa Mbio za Mwenge wananchi wanaombwa wachangie maendeleo yao na kuondosha kero zao kwa kukusanya nguvu zao bila kusubiri serikali.”

Mzee Mwenye alifunga aya alizoeleza kuhusu Mbio za Mwenge kwa kuwashukuru marais wote waliokuja baada yake ya kuendeleza mbio hizo.

error: Content is protected !!