Serikali imeifungia Shule ya Awali an Sekondari ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani kwa muda usiojulikana kwa mujibu wa kifungu cha 4 (8) cha kanuni za mitihani 2016.
Shule hiyo imefungiwa kutokana na taarifa ya Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani pamoja na taarifa ya Wataalam wa Miandiko (Forensic Bureau) kutoka Jeshi la Polisi nchini kubainika kuwa jumla ya watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo PS1408009 shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Octoba 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika kwenye Ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania- NECTA Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Wataalamu wa Miandiko (Forensic Bureau) katika skripti za watahiniwa umebaini kuwa mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0033 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0034 katika somo la sita (mwisho).
Pia, Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0034 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0033 katika somo la sita (mwisho).
Waziri Mkenda amesema kuwa Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0040 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0039 katika somo la sita (mwisho). na Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0039 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0043 katika somo la sita (mwisho).
Vilevile, Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0041 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0040 katika somo la sita (mwisho) na Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0042 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0041 katika somo la sita (mwisho).
“Mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0043 katika masomo matano unafanana na mwandiko wa mtahiniwa PS1408009/0042 katika somo la sita (mwisho)” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa dosari iliyojitokeza katika namba za watahiniwa hao ilisababishwa na uzembe wa watumishi wanne ambao ni Muddy Elphas Mndeme, Msimamizi wa mkondo, Vitalisa Lucas Kindole, Msimamizi Mkuu, Amran Bakari Ramadhani, Mwalimu Mkuu na Rajab Omary Kijangwa, mwalimu wa Takwimu.
Hali kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani umebaini kuwa Mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim alifanya masomo
matano kwa kutumia namba PS1408009/0040 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0039.
Amesema Watahiniwa wengine wanne pia walibadilishiwa namba katika somo la sita (mwisho) ambapo Jasmin Abdallah Mzee alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0041 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0040.
Jokha Abubakar Nassor alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0042 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0041 na Khailat Hamis Mohamed alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0043 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0042.
Prof Mkenda amesema Khaula Khamis Mruma alifanya mitihani mitano kwa kutumia namba PS1408009/0039 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0043.
Waziri Mkenda amewaeleza waandishi wa habari kuwa uchunguzi huo umefanywa kufuatia tukio la tarehe 13/10/2022 ambapo taarifa ilisambaa (Clip) kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika tarehe 05 na 06/10/2022.
Waziri Mkenda amempongeza mwanafunzi Iptisam Suleiman Slim, kwa kutambua na kupigania haki yake na wanafunzi wenzake na kusisitiza kuwa shule yoyote itakayobainika kufanya vitendo vya udanganyifu wa mitihani, itafungiwa na hata kufutwa kabisa kuendesha shughuli za elimu nchini.