Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itafanya uchambuzi wa kina wa mapendekezo 284 ya maboresho ya mifumo ya kodi kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa maboresho hayo yanaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi huku yakipunguza malalamiko kwa walipa kodi.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Mapendekezo ya Maboresho ya Kodi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuyachambua mapendekezo hayo kwa kina kabla ya kuyatekeleza.
Alifafanua kuwa baadhi ya mapendekezo yanahusisha marekebisho ya sheria mbalimbali, maboresho ya taasisi pamoja na uwekezaji wa awali katika mifumo mipya ya ukusanyaji wa kodi.
“Mapendekezo haya yanatupeleka kwenye sera na sheria za kodi zitakazolinda uchumi wetu na kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unakuwa na ufanisi zaidi bila kuongeza gharama,” alisema Rais Samia.
Aidha, alieleza kuwa serikali imepanga kutekeleza mapendekezo hayo kwa awamu tatu; muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, kulingana na uzito na mahitaji ya kila pendekezo.


