Serikali kudahili wanafunzi 500 vyuo vya wenye ulemavu

HomeKitaifa

Serikali kudahili wanafunzi 500 vyuo vya wenye ulemavu

SERIKALI imesema mwaka 2024/2025 imepanga kupitia vyuo vyake vya watu wenye ulemavu kudahili wanafunzi 1500 kati yao wasio na ulemavu ni 500 sawa na asilimia 30 ya wanafunzi wote.

Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ametoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Miriam Nassoro Kisangi , aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuongeza watu wasio na ulemavu kwenye vyuo vya Watu wenye ulemavu.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Mwanaidi, amesema serikali imeandaa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2022-2028 wa Oktoba 2022 na pia inatekeleza Mpango Mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu 2023/24 – 2025/26, ambao pamoja na mambo mengine unahusu suala la elimu na ujuzi kwa kuzingatia ujumuishaji wa watu wenye na wasio na ulemavu katika maeneo ya kujifunza.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwaandaa wanafunzi kuishi maisha jumuishi katika jamii imeandaa mikakati na miongozo hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanajifunza na kuishi katika mazingira yanayowaunganisha na jamii nzima.

“Kupitia Mpango Mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu 2023/24 – 2025/26, Serikali kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 ilipanga kudahili wanafunzi 2,000 kupitia vyuo vya watu wenye ulemavu, kati yao wasio na ulemavu ni 400 hii ni asilimia 20 ya wanafunzi wote.

“Aidha, mwaka 2024/2025 Serikali imepanga kupitia vyuo vyake vya watu wenye Ulemavu kudahili wanafunzi 1500 kati yao wasio na ulemavu ni 500 sawa na asilimia 30 ya wanafunzi wote,” amesema.

error: Content is protected !!