Serikali kununua mahindi ya wakulima

HomeKitaifa

Serikali kununua mahindi ya wakulima

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ametangaza kuwa kuanzia Mei, mwaka huu, serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), itaanza kununua mahindi ya wakulima wa mkoa wa Rukwa kwa bei ya Sh. 500 kwa kilo moja.

Akizungumza na wadau wa kilimo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani Rukwa, alisema serikali itanunua mahindi kwa bei hiyo na kama kuna mfanyabiashara atakwenda kununua, naye atapaswa kuanzia bei hiyo na zaidi ili kulipa thamani zao hilo.

Bashe alisema miaka mingine serikali imekuwa ikianza kununua mahindi Agosti lakini msimu wa mavuno mwaka huu itaanza kununua mapema zaidi kwa kuwa imejenga maghala ya kisasa na mshine za kusafisha na kuyakausha mahindi badala ya kusubiri yakaukie shambani.

Waziri Bashe alisema pamoja na serikali kununua mahindi hayo, pia itaendelea kutoa vibali kuuza mahindi nje ya nchi ili mradi tu mkulima na mfanyabiashara wana uhakika wa soko zuri na afuate taratibu za serikali.

“Serikali yenu inapenda kuona mkulima ananufaika na mazai anayolima ndiyo maana imeweka ruzuku kwenye mbolea. Pia inawezesha maofisa ugani ili wawape elimu, inawatafutia masoko lengo ni kuona maisha ya mkulima yanakuwa mazuri. Niwahakikishie kupitia kilimo safari hii maisha yenu yatabadilika,” alisema.

 

error: Content is protected !!