Serikali yaweka mambo shwari Kariakoo

HomeKitaifa

Serikali yaweka mambo shwari Kariakoo

Hatimaye mgomo wa wafanyabiashara wa Soko la kimataifa la Karikoo wasitishwa mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa maagizo matano yaliyolenga kutatua changamoto zilizokuwepo sokoni hapo.

Waziri Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana Mei 17 na kusisitiza utekelezwaji wa maagizo hayo hususani uvunjwaji wa kikosi kazi cha ukusanyaji kodi.

“Agizo langu la kuivunja task force (kokosi kazi) linabaki pale pale taskforce naivunja, task force hii imeleta watu ambao hawajasomea kodi, imeleta vijana wa kwenye kozi mpya wamekuja na tamaa tamaa zao za maisha.

“Kodi itakusanywa na maafisa wetu wa Mamalakaya Mapato Tanzania (TRA) wamesomea na maadili wakikosea tutawabana kwa taaluma yao,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo juu ya kikosi kazi hicho cha TRA ambacho hukusanya kodi kwa nguvu na kudai rushwa kwa wafanya biashara.

Tozo za stoo kuangalia upya

Akizungumza katika mkutano huo Majaliwa amesitisha kanuni zinazotumika katika ukusanyaji wa tozo za stoo za kuhifadhia mizigo na kuagiza TRA kuziangalia upya ili kubaini maeneo yanayoleta changamoto kwa wafanyabiashara.

“Kuna kanuni hapa ambazo zinaonekana zimetengeneza mianya inayoleta kero, kanuni hizo nazisitisha mpaka hapo zitakapoangaliwa tena upya,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amekemea ukusanyaji wa tozo mara mbili unaofanywa na TRA kwa wafanyabiashara badala ya wanaotunza bidhaa hizo katika stoo zao binafsi.

“Najua biashara mnazobeba jioni hamrudi nazo huyo na yeye anatakiwa kulipa na siyo nyie…kama stoo haina kero kwanini kero ije kwenye stoo ya wafanyabiashara,” amehoji.

Aagiza mizigo iliyozuiwa kupunguziwa kodi

Kukamatwa kwa mizigo ya wafanyabiashara nchini ni changamoto nyingine iliyolalamikiwa sana katika mkutano huo ambapo Waziri Mkuu ameagiza kuachiwa kwa mizigo hiyo kwa uratibu maalumu pamoja na kupunguziwa kodi.

“Hii mizigo itoke kwa utaratibu…kama kero ilikuwa na ukubwa wa kodi kamishna wa TRA ana sheria inamruhusu pia  kurekebisha rekebisha masuala ya kodi.

Kamishna wa TRA mizigo imekaa sana mingine imepoteza thamani mingine inataka kuoza uking’ang’ania kulipwa ileile hutapata chochote itaharibika…au achia kabisa,”  amesisitiza.

Yaliyolalamikiwa na wafanyabiashara

Awali wafanyabiashara katika soko hilo la kimataifa waliibua malalamiko mbalimbali ambayo kwa kipindi kirefu yamekuwa kero yakiwazuia kufanya biashara zao kwa uhuru.

Moja kati ya mambo yaliyolalamikiwa ni utitiri wa kodi jambo ambalo linaathiri biashara zao ambapo wameshauri kuwe kuna kodi moja tu inayojumuisha kodi nyingine kuliko kila taasisi kuwa na kodi yake kama ilivyo sasa.

“Miongoni mwa marekebisho ni tuwe na makapu mawili au matatu bandarini, manispaa na TRA ukikadiriwa kule ukilipa huku utoe risiti usitoe kodi umeshalipa, hii itatusaidia na mtapata hela nyingi madukani,” amesema Dismas Massawe ambaye ni mfanyabiashara kutoka Singida

Ushuru  wa huduma kaa la moto

Ismail masoud ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara mkoani Tanga amemwambia Waziri Mkuu kuwa kodi ya huduma (Service Levy) imekuwa chanzo cha wafanyabiashara wengi kufilisika kwa kuwa hawakadiriwi kiwango sahihi cha kodi kutokana na kodi hiyo kujikita kwenye fedha iliyopatikana baada ya mauzo na sio faida halisi.

Kodi hiyo  ni matokeo ya Sheria ya fedha namba 9 ya 1982 kifungu cha 6 (1)(U). ambayo  hulipwa na makampuni, taasisi na biashara mbalimbali zilizosajiliwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kutokana na mauzo ghafi kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3.

Kwa kawaida kodi hii hukusanywa mara nne kwa mwaka kila baada ya miezi mitatu ambapo mlipakodi huwasilisha mauzo yake kwa wataalamu wa kodi ambao hukokotoa kiasi kinachotakiwa.

Kodi za miaka mitano iliyopita

Kupuuzwa kwa agizo la Rais la kusamehe kodi za miaka mitano iliyopita kumewaibua tena wafanyabiashara ambao wamemwambia Waziri Mkuu kuwa maafisa wa TRA wamekuwa wakiwataka watoe barua kutoka kwa Rais kuthibitisha madai hayo.

“Wakifika wanasema zile ni kauli za kisiasa, hakuna mfanyabiashara ambaye hajaumizwa hapa, ni vijana wadogo wadogo wanakwambia tupe barua ya Rais, yale alitamka tu akiwa jukwaani,”  amesema mfanyabiashara huyo.

Baadhi ya masuala mengine yaliyolalamikiwa kiujumla ni pamoja na kukosekana kwa elimu kodi kwa wafanyabiashara, kupitisha sheria za kodi bila kupokea maoni kwa wafanyabiashara, urasimu wa baadhi ya maafisa wa TRA pamoja na baadhi ya maafisa wa polisi kuingilia masuala ya kodi na kuchukua rushwa.

Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamekutana na Waziri Mkuu wa Tanzania kujadili changamoto zinazowakabili kufuatia mgomo wa siku mbili, ambapo wamealikwa wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali kuelezea changamoto za kikodi zinazowakabili.

Waziri Mkuu ameambatana na mawaziri wa kisekta akiwemo Waziri wa Fedha  Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni ambao wanasikiliza changamoto zinazotajwa na wafanyabiashara hao ili kuzifanyia kazi.

Mazungumzo haya yanakuja baada ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kugoma kufungua maduka yao kwa siku tatu mfululizo wakigomea utekelezaji wa kodi ya ghala, kamata kamata ya wafanyabiashara pamoja na ushuru wa forodha.

error: Content is protected !!