Serikali imetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira, ujasiriamali na ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema fedha hizo zitatumika kuwezesha vijana kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi kupitia programu maalum itakayotekelezwa kwa kushirikisha taasisi mbalimbali za serikali.
“Serikali imetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi,” alisema Waziri Omar wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 bungeni.
Hatua hiyo inakuja wakati vijana wakiendelea kuwa sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini, huku Serikali ikiongeza juhudi za kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na uanzishaji wa biashara.
Mpango huo unatarajiwa kusaidia vijana kupata mitaji, mafunzo ya ujasiriamali na fursa za kuunganishwa na masoko, sambamba na jitihada za Serikali za kukuza uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi wa makundi yote.
Uwezeshaji wa vijana ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2026/27, huku Serikali ikieleza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza ajira, kipato na tija katika sekta mbalimbali za uchumi.


