Kodi mpya kwa mafuta ghafi ya kula yanayoingizwa nchini

HomeKitaifa

Kodi mpya kwa mafuta ghafi ya kula yanayoingizwa nchini

Serikali imependekeza kuanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwa mafuta ghafi ya kula ya aina mbalimbali yanayoingizwa nchini, ikiwemo mafuta ya mchikichi pamoja na yale yaliyopitia uchakataji wa awali.

Akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano yaliyohusisha wadau wa sekta ya mafuta ya kula, wazalishaji na kamati mbalimbali za Bunge.

Serikali inaamini hatua hiyo itasaidia kuweka uwiano katika ushindani wa biashara ya mafuta ya kula na kuimarisha usimamizi wa bidhaa zinazoingizwa nchini.

Ameeleza kuwa ushuru huo unalenga kukabiliana na vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara kutumia vibaya tofauti za viwango vya ushuru kwa kuainisha mafuta yaliyosindikwa kama mafuta ghafi ili kupata nafuu ya kodi.

Amesema kiwango hicho cha ushuru kinaendana na utaratibu unaotumiwa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya na Uganda, ambazo tayari zinatoza ushuru wa asilimia 10 kwa mafuta ghafi ya mchikichi yanayoagizwa kutoka nje ya jumuiya hiyo.

error: Content is protected !!