Sh3 bilioni kutumika Samia Scholarship

HomeKitaifa

Sh3 bilioni kutumika Samia Scholarship

Jumla ya Sh3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi katika mitihani yao ya kidato cha sita.

Ufadhili huo ambao unaanza mwaka 2022/2023 unafanyika chini ya mpango unaojulikana kama Samia Scholarship.

Akizungumza hayo leo Jumapili Septemba 25,2022, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Septemba 27,2022 wanafungua rasmi tangazo la ufadhili huo ambao utawahusisha wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha juu na kudahiliwa kusoma masomo ya sayansi katika vyuo mbalimbali.

“Baada ya hapo majina yao yatatanangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa wamefanya vizuri sana katika masomo ambao wanastahili kupewa Mama Samia Scholarship,”amesema.

Amesema kuwa wanafunzi 640 ndio waliofaulu kwa kiwango cha juu katika masomo ya sayansi, kwa hiyo watafahamu na endapo watadahiliwa katika masomo ya sayansi watakuwa wanufaika wa ufadhili huu.

Aidha, Profesa Mkenda amesema kesho kutakuwa na mkutano wa wadau wa elimu nchini ambapo lengo likiwa ni kupitia sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na mabadiliko ya mtaala wa elimu.

“Majadiliano yatatokana na hatua iliyofikiwa kutokana na mapitio ya sera na mitaala baada ya kukusanya maoni mengi ya wadau ambayo tuliyakusanya kupitia mikutano mbalimbali na wengine wamekuwa wakituletea kimaandishi,”amesema.

Amewataja wadau watakaokutana ni wahadhiri, waajiri na wadau wa maendeleo, taasisi zinazohusihanisha na lugha, wabunge, wajumbe wa kutoka Zanzibar, jumuiya za kielimu, taasisi za tafiti za kisayansi, taasisi za umma, binafsi na dini.

Pia Profesa Mkenda amewataka Watanzania kuwasilisha rasimu za maandiko yao za riwaya na mashahiri katika kuwania tuzo za waandishi bunifu ambazo zinajulikana kama tuzo za Mwalimu Nyerere.

error: Content is protected !!