Shaka: Tanzania tunaye muongoza njia

HomeKitaifa

Shaka: Tanzania tunaye muongoza njia

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amewataka viongozi wa Chama na serikali kuwashirikisha vijana katika mipango ya maendeleo, kwani Rais Samia Suluhu Hassan, amewekeza nguvu kubwa kuliinua kundi hilo kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zilizopo nchini.

Amesema CCM kinaamini vijana wakiwezeshwa kiuchumi wanauwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa kwa kiwango kikubwa zaidi na ilivyokuwa sasa.

Shaka aliyasema hayo jijini hapa jana wakati akizundua ujenzi wa nyumba ya mshindi wa kwanza atakayepatikana katika mashindano ya mbio za waendesha bodaboda kitaifa, yanayotarajiwa kuhitimishwa Agosti 30 mwaka huu yakiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kutangaza fursa za utalii nchini kupitia filamu ya Royal Tour.

“Tanzania tunaye muongoza njia, mfungua fursa ambaye ni Rais Samia mwenye kutekeleza dhana na maono ya kuwakomboa vijana kiuchumi kupitia fursa na rasilimali zilizopo nchini, Rais Samia amefanya uwekezaji mkubwa katika kuwainua vijana.

Alisisitiza kuwa: “Jitihada hizi zinapaswa kuendelea kuungwa mkono kwa viongozi wa Chama na serikali kuwashirikisha vijana katika mipango ya maendeleo. Hii itasaidia kutekeleza kwa vitendo ahadi ya CCM ya kutoa ajira milioni nane kwa sekta rasmi na zisizokuwa rasmi.”

Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi alieleza kuwa CCM kinaamini kwamba endapo vijana wakiwezeshwa zaidi kiuchumi, watachangia maendeleo ya taifa kwa hatua kubwa zaidi na ilivyokuwa sasa. 

Alibainiaha kuwa  mbio hizo za waendesha bodaboda ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo pamoja na waendesha vyombo hivyo vya moto kuwa mabalozi wazuri wa utalii.

Shaka alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wandesha bodaboda na bajaji kushiriki Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu pamoja na kuendelea kupata chanjo ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Uviko-19.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Global Peace Advocacy for Conflict Resolution, Ryamoja Mfuru, alisema taasisi hiyo imeandaa mashindano hayo kuwawezesha waendesha bodaboda kubeba ujumbe wa kuhamasisha utalii nchini.

Alieleza kuwa mbio hizo ngazi ya wilaya zitaanza Agosti 13 mwaka huu kisha Agosti 17 zitaendelea kwa ngazi ya mkoa na kuhitimisha kitaifa Agosti 30 mwaka huu ambapo mshindi atakabidhiwa nyumba iliyopo jijini Dodoma.

Naye, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga, alisema CCM kimekuwa na ushirikiano mzuri na Umoja wa Waendesha Pikipiki Mkoa wa Dodoma (UWAPIDO) ambapo imetoa ofisi kwa ajili ya uendeshaji shughuli za chama hicho.

Mwakilishi kutoka kampuni ya State Aviation, Amour Abdallah, alisema kampuni hiyo itatoa helkopta kuhamasisha tukio hilo kwani uwezeshaji vijana hususan madereva bodaboda ni msaada muhimu katika kuchangia maendeleo ya taifa.  

error: Content is protected !!