Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa miezi miwili kufanyika tathmini ya madhara ya shisha kabla ya Serikali kuchukua uamuzi ya kuipiga marufuku na kuijumuisha miongoni mwa madawa ya kulevya.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC), shisha ni kifaa ambacho tumbaku huwekwa ndani ya bakuli na kuwashiwa moto ili kutoa moshi kupitia kiriba ambacho huipoza na kisha kuingizwa kwenye mirija ambayo huto moshi unaovutwa na watu kwa kutumia mdomo.
Ummy Ametoa maagizo hayo kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Tume ya Madawa ya Kulevya Tanzania kufanya tathmini hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani jana Mei 31, 2022 jijini Dodoma yenye kauli mbiu isemayo “Tumbaku:Tishio kwa Mazingira Yetu”.
Licha ya sheria za Tanzania kukataza uzalishaji na usambazaji wa baadhi ya bidhaa za tumbaku kama shisha, ugoro na sigara za kielektoniki bado bidhaa hizo zipo na zinaendelea kutumiwa na wananchi hasa vijana.
“Tunafahamu shisha zipo katika mahoteli mengi makubwa hususani Dar es Saalam, nilichowaelekeza ni kufanya tathmini ya bidhaa hizi ili kuona namna ya kupunguza au kusitisha matumizi ya bidhaa hizi,” amesema Ummy.
Muda huo wa miezi miwili uliotolewa hautoi msamaha kwa wazalishaji na wasambazaji wa bidha hizo, kwani Sheria ya Kudhibiti Bidhaa za Tumbaku ya sura ya 121, inasema uzalishaji usambazaji na utumiaji wa bidhaa hizo ni kosa kisheria.
“Kama mtu anafanya biashara ya Shisha ajue kwamba ni kinyume cha sheria, ajue kwamba nafanya kosa la jinai,” amesisitiza waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Tanga mjini.
Uamuzi huo wa Waziri Ummy umekuja baada ya kuwepo madai kuwa shisha inachanganywa na dawa za kulevya na kuongeza madhara kwa watumiaji wake, hivyo kuna umuhimu wa kufuatilia kwa karibu suala hilo.
Mbali na tafiti za dunia kuhusu athari za bidhaa zitokanazo na tumbaku, watu 14,700 hupoteza maisha nchini Tanzania kutokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.