Kauli ya RC Makalla siku 3 kabla ya zoezi la kuondoa machinga

HomeKitaifa

Kauli ya RC Makalla siku 3 kabla ya zoezi la kuondoa machinga

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makalla amewataka wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga kutumia vizuri siku tatu zilizosalia kuhamia kwenye maeneo waliopangiwa kwani ifikapo Oktoba 18, 2021 kila mfanyabiashara anatakiwa kuwa kwenye eneo alilopangiwa.

Wafanyabiashara wanaotakiwa kuhama ni wale wote wenye vibanda vya biashara juu ya mitaro ya maji, wanaofanya biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, wanaofanya biashara kwenye hifadhi za barabara, wanaofanya biashara mbele ya maduka na wanaofanya biashara kwenye taasisi za umma.

> Makalla ataja maeneo matano watakayoanza kuwaondoa Machinga

Sambamba na hilo wafanyabiashara wote wenye meza za biashara katikati ya barabara za mitaa ya Kariakoo na Msimbazi wanatakiwa kuondoka ili kuhakikisha barabara hizo zinabaki wazi. Mkuu wa Mkoa Makalla amesisitiza kuwa Serikali itatumia siku tatu zilizobaki kuongeza matangazo na elimu kwa wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wadogo wanatakiwa kwenda kwenye maeneo rasmi ili kupunguza changamoto kama za watu kugongwa na magari kwasababu ya kukosa sehemu ya kupita pamoja na usalama wa wafanyabiashara hao. Vilevile Mhe. Makalla amewataka madereva daladala kushusha abiria katika maeneo hayo ya masoko ili kuchochea kukua kwa biashara katika maeneo yaliyotengwa maalum kwa wafanyabiashara hao.

error: Content is protected !!