Simulizi ya maisha ya Zacharia Hans Poppe (kufungwa gerezani hadi kiongozi wa Simba)

HomeMichezo

Simulizi ya maisha ya Zacharia Hans Poppe (kufungwa gerezani hadi kiongozi wa Simba)

 

Zacharia Hanspope amelazwa kwenye nyumba yake ya milele kijijini kwao Kihesa Iringa, ambapo baba yake mzazi pia alizikwa miaka 42 iliyopita.

Septemba 10, kifo cha Zacharia Hans Poppe kilitangazwa. Mwanasimba huyo mwili wake uliagwa kwa heshima siku ya Jumatatu na Jumapili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hans Poppe, alitajwa kama mtu rahimu, mpole na msikivu kwenye kazi zake, hasa ndani ya bodi ya wakurugenzi wa Simba.

Wengi walifahamu Hans Poppe kama mfanyabiashara na mwanasimba kindakindaki. Lakini Zachakari ana ukurasa katika maisha yake ambao pengine wengi hawajawahi kuufunua. Hans Poppe alikuwa mpiganaji, ni moja ya watu waliosimama mstari wa mbele kupigana wakati wa vita ya Kagera mwaka 1978. Wakati wa vita Zacharia alikamatwa, akiwa yeye na Kaka yak aitwaye Harry, wote waliwekwa gerezani lakini kwa mafunzo waliokuwa nayo waliweza kutoroka gerezani na kuendeleza mapingano hadi nguli Idi Amin Dada anang’oka madarakani.

Ni kwa uchache sana kisa hiki cha Zacharia kinaelezwa kwa undani, lakini haiba ya upole na usikuvu aliyokuwanayo Hans Poppe ingeweza kukudanganya kama utapata kusikia upande wa pili wa shilingi wa maisha yake. Zacharia kabla ya kwenda vitani 1978, mzimu wa madhila ulianza kuandama maisha yake miaka 8 nyuma wakati Baba yake mzazi, Mzee Hans Poppe, alipouawa na Jeshi la Uganda mkoani Kagera ambapo alikuwa akifanya kazi kama Polisi.

Haikutosha kwa Jeshi la Uganda kumuua tu Mzee Hans Poppe, bali walichukuwa mwili wake hadi Uganda na kuuweka katika Hospitali ya Mulago kwa miaka 8, mwili ukiwa umefungashwa kama rumbesa katika majokofu ya Hospitali hiyo. Hadi 1979, baada ya Jeshi la Tanzania kuvamia kampala wakati wa Vita ya Kagera, na kuuchukua mwili huo na kurudishwa Tanzania kwa maziko ya heshima.

Miaka minne baada ya kumalizika kwa vita ya Kagera, mzimu wa majanga bado uliendelea kuandama maisha ya Zacharia, yeye na kaka yake wakatiwa hatiani kwa makosa ya uhaini.

Ilikuwaje?

Wakati Tanzania inakusanya nguvu kujinasua kutoka kwenye hasara na matatizo yaliyosababishwa na vita vya Kagera, hali ya uchumi haikuwa nzuri, maisha kwa kiasi kikubwa sana yalikuwa magumu sana. Mwaka 1983, kutokana na hali hiyo, walitokea watu ndani ya Jeshi la Tanzania ambao walishindwa kabisa kustahalimi hali hiyo na kuamua kuchukua hatua ya kutaka kupindua Serikali. Mkasa wote huu kabla ya vita na baada ya vita unaelezwa vyema kabisa na Godfrey Mwaikikagile kwenye kitabu chake cha “Nyerere & Africa: End of an Era” ambapo ndani yake Zacharia binafsi anatoa ushuhuda wake juu ya mkasa huo.

Zacharia anasemea, … “Mwaka 1983 hali ya uchumi wa Taifa letu haikuwa nzuri hata kidogo, maisha yalikuwa magumu sana kiasi cha kushindwa kuvumilia, na kwa wakati huo, ni ngumu sana kufanya mabadiliko kwa njia ya maongezi, ilitupasa tutumie nguvu,” aliongeza Zacharia.

Jaribio zima la mapinduzi lilipangwa na Pius Mtakubwa Lugagira kuanzia Novemba 1982 na likafanyika Januari 1983. Jaribio hilo lilishindwa kufua dafu kutokana na mpango mbovu kwa kuwa wakati wanapanga tayari makachero wa Nyerere walishapata taarifa za Kiintelijensia kuhusu mpango huo.

Kukamatwa kwa Hans Poppe
Siku ya tarehe 7 Januari 1983 majira ya saa 9 alasiri, watu waliopanga mapinduzi walikuwa maeneo ya Kinondoni wakiingia kwenye nyumba kadhaa kupanga mashambulizi ya siku ya pili.

“Nilikuwa karibu sana wakati namuona Mohammed Mussa Tamim akifukuzwa na watu watatu, na ghafla nikasikia milio ya risasi na Tamimu alianguka kifudifudi baada ya kupatwa na rasasi wakati akijaribu kutoroka kwa kudandia gari iliyokuwa inatembea,”.. Zacharia alisema.

Tamimu ni moja ya watu waliopanga jaribio la mapinduzi na aliuawa na makachero wa Serikali. Mwili wake ulipelekwa Mochwari, na Zacharia aliamua kuenda hadi Hospitali kushuhudia nini kitafuata baada ya mwili wa Tamimu kufika mochwari. Zacharia alipofika mochwari alitoa hongo kidogo kwa mhudumu wa zamu ili ampe ruhusa ya kuingia mochwari. Muhudumu yule alimwambia Zacharia kauli ambayo ilimtisha sana, alisema, “Makachero walioleta mwili wa Tamimu walikuta karatasi ndogo mfukoni mwake ambayo ina orodha ya majina ya askari jeshi wenye vyeo vya juu.”

Bila kujua Zacharia alikimbia kurudi Kinondoni, alipofika alikuta tayari nyumba yake imezingirwa na askari kila kona. ..”Nilikuta tayari kuna wenzangu wako kizuizini huku askari wakizunguka uzio wa nyumba yangu kuangalia kama kumefichwa silaha.”

Hakuwa na chakufanya kabisa, na tayari ilikuwa majira ya saa mbili usiku. Kuanza hapo, kila mtu alianza kutetea roho yake, kwani ndio mpango wote ulivurugika hapo.
Kuna baadhi ya wenzake walikimbilia Kenya wakapewa hifadhi huko, na Zacharia alikuwa tayari ameoa na ana mtoto mmoja, aliamua kubaki apambane hadi mwisho.

Alipofikishwa Central alimkuta kaka yake Harry, (Harry ni Kapteni na pia ni rubani). Harry alikamatwa awali kwasababu alikuwa anaishi kwenye kambi za wana anga, hawakujua Zacharia anaishi wapi hivyo walilazimika kumkamata Harry hadi aseme Zacharia anaishi wapi.

Siku ya Pili Zacharia alichukuliwa na askari hadi nyumbani kwakwe na kupekuliwa lakini hakukutwa na kitu, na baadaye alipelekwa kupekuliwa kwenye ofisi yake ambapo pia hakuna kilichopatikana.

Watu 30 ambao ni wanajeshi walioshiriki jaribio walikamatwa na kupelekwa Ukonga, na raia walipelekwa gereza la keko. Waliopelekwa Mahakamani na Zacharia ni Luteni Colonel Martin Ngalomba, Kapteni Suleiman Metusela, Luteni Kanali Martin Peter Msami, Meja Reverian Bubelwa, Kapteni Vitalis Gabriel Mapunda and Kapteni Dietrich Oswald Mbogoro.

Mahakamani, Zacharia Hans Poppe, Tamimu na washitakiwa wote, walishitakiwa kwa kosa la kutaka kumuua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius Nyerere ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu. Pamoja na hayo, pia walishitakiwa kwa kutaka kupindua Serikali.

Kesi ya uhaini ya akina Hans Poppe ni kesi ya pili ya namna hiyo Tanzania bara baada ya ile ya mwaka 1970 ambayo ilisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Ingawa, kesi ambayo ilikuwa inawakabili watu 30, ilifutwa siku chache baadae tarehe 17 Juni 1983 baada ya watuhumiwa watu, Pius Mutakubwa Lugangira na Hatty McGhee kutoroka mahabusu na kutokomea.

Pius na Hatty walikimbilia Kenya, lakini Tanzania ilikuwa inamshikilia Mkenya Hezekia Rabala Ochuka ambaye Serikali ya Kenya ilikuwa inamtaka sana. Serikali hizi mbili zikakubaliana kuwa wabadilishane wahalifu, Tanzania akarudishwa McGhee na Kenya wakapewa Hezekia.

Kesi ikanguruma kwa miezi 7 baadaye watuhumiwa wanne kati ya 19 waliobaki wakakutwa hawana hatia na kuachiwa 1985. Decemba 1985 Jaji Mzava alisema kuwa kulikuwa na jaribio la Mapinduzi ya Serikali, na kati ya 19, 9 walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha akiwamo Zacharia, na waliobaki kuachiwa huru.

Zacharia alisema kuwa wakati yuko Gerezani alichukuliwa kama mfungwa wa kisiasa. Alipewa huduma zote kama magazeti, kusikiliza redio, chandaru, chakula, maji, kitanda kizuri cha kulala na hata kutembelewa na ndugu na jamaa zake katika kipindi cha takribani miaka 13 alichokaa gerezani. Na kipindi chote hiko akitumikia katika magereza tofauti kama Ukonga, Maweni, Lindi na Mtwara Kabla ya kuachiwa huru kwa msamaha wa raisi mwaka 1995.

Maisha baada ya Jela

Hans Pope alipotoka gerezani ilikuwa ngumu sana kukubalika kwenye jamii. Hans Poppe alikuta ametalikiwa na mkewe na ameolewa na mtu mwingine. Hans Poppe alikaa miaka 6 na yeye kuoa mwaka 2001.

Wana habari za michezo wanasema kuwa Hans Poppe alipenda sana michezo tangu akiwa kijana na alijiunga na Simba miaka ya 70.

error: Content is protected !!