Soko la machinga kujengwa Kigogo, Dar kupunguza msongamano Kariakoo

HomeKitaifa

Soko la machinga kujengwa Kigogo, Dar kupunguza msongamano Kariakoo

Serikali imesema itajenga soko jipya la Machinga katika eneo la Kigogo Sambusa, kwa lengo la kupunguza msongamano na kutatua kero za muda mrefu zinazokabili wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo.

Akizungumza leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe katika kikao cha pamoja na viongozi wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Wamachinga na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema hatua hiyo inalenga kutoa ahueni ya haraka kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara Kariakoo, wakati Serikali ikiendelea na mipango ya kukamilisha mradi mkubwa wa soko la kudumu unaohusishwa na uendelezaji wa Bonde la Msimbazi.

“Lengo la Serikali ni kupunguza msongamano uliopo Kariakoo. Ujenzi wa tuta katika eneo la Kigogo Sambusa unaanza mara moja na ukikamilika, Halmashauri ya Jiji la Ilala itaanza ujenzi wa soko. Tunataka eneo hili liwe tayari ili Wamachinga waweze kuhamia na kufanya biashara zao kwa amani,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amesema mradi wa soko hilo utagharamiwa kupitia asilimia tano (5%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Ilala, hivyo amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia sheria ya kuruhusu mapato ya asilimia tano (5%) ya ndani yaliyolindwa yatumike kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu ya biashara ikiwemo ujenzi wa masoko.

error: Content is protected !!