Kufufua Shirika la Ndege Tanzania ilikuwa ni moja ya ndoto ya Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Wakati wa uhai wake, Tanzania ilishuhudia ikipokea ndege mpya 8 hadi kufikia Oktoba 2019, ndege hizo 4 ni Bombadier, Dash 8 Q-400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Boeing 787-800, Dreamliner 2 zenye uwezo wa kubeba abiria abiria 262 kila moja pamoja na Airbus A200-300 mbili. Baada ya Rais Magufuli kufariki na Rais Samia Suluhu Hassan kushika madaraka, ndege mpya ya 9 aina ya Bombadier Dash 8 Q-400 ilipokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 30, Julai 2021 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere.
Kati ndege 11 ambazo Serikali ya Tanzania ilidhamiria kununua, zote zimeshawasili huku 8 zikipokelewa na hayati Dkt. Magufuli, 1 ikipokewa na Rais Samia Suluhu Hassan na 2 zikipokelewa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 8 Oktoba 2021.
Mapokezi ya ndege 9 kati ya 11 yalifanyika Tanzania Bara, 7 zikipokelewa Uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam, na 1 aina ya Bombardier Q400 ikipokelewa, Mwanza Disemba 14, 2019 na Rais John Pombe Magufuli mwenyewe. Sote tunafahamu kuwa Tanzania imetokana na muungano wa nchi mbili kati ya Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Baba wa Taifa, (Tanganyika), Mwl. Julius Nyerere na Sheik Abeid Karume (Zanzibar) tarehe 26 Aprili 1964 punde baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ni swali ambalo mtu anaweza kujiuliza akakosa majibu ya kuridhisha, lakini kwa sababu tuko katika nchi ambayo kikatiba inatoa uhuru wa kutoa na kuchangia mawazo, basi ni aula sana kuja na tafakuri kama hizi ili kujaribu kutoa majibu ambayo yatafungua mafundo ya maswali katika vichwa vyetu. Zipo sababu kadhaa ambazo naona zimepelekea ndege 9 kupokelewa Tanzania bara na 2 za mwisho kupokelewa visiwani Zanzibar.
Sababu ni kama zifuatazo:
- Suala la usafiri wa anga ni jambo la Muungano
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni muungano wenye heshima kubwa duniani. Kwanza ni moja kati ya muungano imara na uliodumu muda mrefu bila machafuko wala vurugu, hivyo basi muungano huu kulingana na heshima na umuhimu wake utalindwa na kudumishwa kwa hali yoyote. Muungano wetu una mambo 22, kati ya mambo hayo jambo la 11 linahusu bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu’. Tafakuri yangu inanambia kuwa, kama suala la anga ni jambo la muungano, isingependeza kama ndege zote zingepokelewa Bara, hivyo basi ili kila Mtanzania ahisi fahari ya utanzania wake, hakuna budi awe sehemu ya kushudia historia ya Taifa lake hasa kutumiza malengo makubwa kwa maslahi ya watu wake. Serikali imepiga mahesabu mazuri kwenye hilo, mahesabu yenye kulenga kujenga utaifa, umoja pamoja na mshikamo ambao utalinda na kutunza Muungano wetu.> Fahamu sifa za ndege ya Airbus A220-300
- Ndege kupewa jina la Zanzibar
Kati ya ndege mbili zilizopokelewa visiwani Zanzibar, ndege moja imepewa jina la Zanzibar. Ndege hizi ni ndege za masafa marefu kwa mujibu wa maelezo ya Serikali, hivyo kupewa jina la Zanzibar zitatangaza utalii wa Zanzibar, hivyo imependeza zaidi ndege hizo kupokelewa Zanzibar kuliko sehemu nyingine. Hii haina maana kila ndege inayojpewa la mahali fulani, ni lazima ipokelewe eneo hilo, la hasha. Ila kwenye hili tafakuri yangu inanambia kuwa isingependeza sana ndege yenye jina la Zanzibar kutua kupokelewa Tanga au Dodoma. Isingedhuru kama zingepokelewa maeneo tofauti na Zanzibar, lakini kutia utamu zaidi kwenye mapokezi, Ndege yenye jina la Zanzibar kutua Zanzibar basi utamu zaidi.
- Kumpa heshima Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi
Kusingalikuwa na Tanzania kama sio Zanzibar, hivyo basi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni mtu muhimu sana kwenye ustawi wa Taifa letu. Rais Magufuli alishapokea ndege 7, huku Rais Samia akiwa kama makamu wake, baadae Mh. Samia alipokuwa Rais naye akapokea 1. Ilibakia Rais Mwinyi pekee ambaye ni mhimili wa Muungano wetu kwa upande wa Zanzibar kupokea ndege. Tafakuri yangu inanambia kuwa upo umuhimu wa kumpa heshima Rais Mwinyi kutokana na umuhimi mkubwa aliokuwa nao kwenye taifa hili. Sina Hakika sana, ila nadhani Rais Samia hakushindwa kusafiri kwenda Zanzibar kupokea ndege, lakini tafakuri yangu inanambia kuna busara ya hali ya juu imetumika hapa ili kumpa heshma Dkt. Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.