Tahadhari kirusi kipya

HomeKitaifa

Tahadhari kirusi kipya

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema serikali inafuatilia uwapo wa aina mpya ya kirusi cha UVIKO-19 kilichothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kinachojumuisha kirusi cha Delta na Omicron, ambacho kimejiunda na kuwa kirusi kipya cha Omicron BA.1.

“Nimeshawaelekeza wataalamu wetu waangalie tuone kama kimeshaingia nchini kwetu kwa sababu nchi nyingine wameshathibitisha,” alisema Waziri Ummy.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Waziri Ummy aliwasihi Watanzania kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga na kirusi hicho na kusema endapo watu wengi watapata chanjo itasaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huo.

Aidha, alisema hali ya uchanjaji bado ipo chini nchini kwa sababu asilimia 66 ya wanaougua UVIKO-19 waliolazwa hospitalini hawajapata chanjo, hali ambayo ni hatari kwa nchi na kusisitiza umuhimu wa Watanzania kujikinga na ujio wa kirusi hicho.

error: Content is protected !!