Tanzania na Hungary kuangazia usawa wa kijinsia

HomeKitaifa

Tanzania na Hungary kuangazia usawa wa kijinsia

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake inalitizama kwa jicho la tatu suala la usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake katika jamii.

Rais Samia amesema hayo leo Julai 18, 2023 Ikulu, Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari katika mapokezi ya Rais wa Hungary Katalin Novak katika ziara ya Rais huyo nchini.

Katika mkutano huo Rais Samia amesema Tanzania na Hungary wapo katika mpango mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na kusema amefurahishwa na maono ya Rais wa Hungary, Katalin Novak katika masuala ya usawa wa Kijinsia.

“Katika majadiliano yetu tumekubaliana kuweka mbele masuala ya jinsia, ninataka kukushukuru Rais kwa kulipa kipaumbele pia suala hili kwa sabu katika serikali yangu ni moja ya ajenda muhimu,“ amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais wa Hungary Katalin Novak, amesema ni furaha kubwa kwake kufika Tanzania na kilichomfurahisha zaidi ni kukutana na kiongozi mwenzake wa ngazi ya juu mwenye jinsia ya kike kitu ambacho kinawapa jukumu la kuhamasisha zaidi mabinti kupigania ndoto zao.

“ Hawapaswi kukata tamaa kwenye kile wanachokiamini ama ndoto zao lakini pia kutokata tamaa juu ya jukumu lao la kuwa mama na kufanikiwa katika taaluma zao , kwahiyo tunataka kuwapa moyo wanawake wote,” amesema Rais Katalin.

error: Content is protected !!