Ukurasa mpya ndiyo unavyoweza kusema baada ya Tanzania na Zambia kufufua upya uhusiano wa kindugu na ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo baada ya kufifia kwa takriban miaka sita iliyopita.
Tangu mwaka 2016 mahusiano kati ya mataifa haya jirani hayakuwa ya kuridhisha, jambo lililofanya yashindwe kufaidika na fursa zinazopatikana pande zote mbili.
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na vyombo vya habari jana Agosti 2, 2022 Ikulu jijini Dar es salaam amesema wamekubaliana na Rais wa Zambia Haikande Hichilema kuyarejesha mahusiano ya kindugu yaliyoanzishwa na waasisi wa mataifa haya mawili.
Rais Samia amesema Hayati Julius Nyerere na Kenneth Kaunda, mwasisi wa Taifa la Zambia waliweka misingi ya ushirikiano na kuanzisha mambo ambayo walitaka yadumu milele lakini kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yamesababisha kumekuwa na umbali baina ya nchi hizo mbili.
“Mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na kisiasa kwenye ulimwengu yametufanya kidogo tumetengeneza umbali baina yetu tumekubaliana na ndugu yangu Hichilema turudishe ule udugu wetu kama tulivyoachwa na wazazi wetu,” amesema Samia.
Rais samia amesema bila kujali yaliyotokea ni muhimu viongozi wa mataifa haya mawili wakawaongoza wananchi waelewane vizuri ili kukuza umoja utakaowaleta karibu kufaidiana katika mambo mbalimbali.
Pia ushirikiano huo utajikita zaidi katika sekta ya miundmbinu ya usafirishaji ikiwemo kuiboresha reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na bomba la mafuta la Tazama ili kuchagiza uchumi wa nchi hizo mbili.
“Tumekubaliana kuwa na mradi wa pamoja tutafute fedha pamoja kupitia ushirikiano na sekta binafsi na marafiki waliotujengea hiyo reli tuone tunavyoweza kuiboresha kwenye kiwango cha reli ya kisasa.
“Tumekubaliana kujenga bomba kubwa litakalopeleka mafuta mengi zaidi na bandari ya Dar es salaam na miundombinu iliyopo Tanzania iwasaidie kupunguza ughali wa mafuta katika nchi yao,” amesema Rais Samia.
Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji
Licha ya kuwepo kwa mahusiano na muingiliano wa kibiashara na uwekezaji baina ya wananchi wa mataifa haya mawili bado kumekuwepo na vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi ambavyo vinakwamisha ukuaji wa biashara.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Rais Samia amesema wamekubaliana kuwa sekta za uwekezaji na biashara, taasisi za mapato za mataifa yote mawili kukaa na kutazama vikwazo vinavyotukabili ili viondolewe.
“Hapo hapo kwenye biashara tumewazungumzia wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanapovuka mipaka yetu kwenda kufanya biashara masharti wanayopewa ni makubwa kwa hiyo tumesema mawaziri wetu wakae na waangalie jinsi ya kusaidia,”amesisitiza Rais.
Nishati na kilimo
Ili kuimarisha upatikanaji wa nishati mataifa haya Samia amesema wamekubaliana kutekeleza mradi wa pamoja wa umeme ambapo Tanzania itaanza utekelezaji wake Januari 2023.
Rais Hichilema amesema ushirikiano na undugu ulioanzishwa na waasisi wa mataifa haya ni urithi ambao unapaswa kulindwa na kumwagiliwa kila siku ili uzidi kukua.
Amesema yeye na Rais Samia atahakikisha wanaongeza faida za ushirikiano wa mataifa hayo ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali zinazowazunguka kama Ziwa Tanganyika.
“Tumechaguliwa na wananchi ili kuboresha maisha yao, tunatakiwa kushirikiana ili kuinua uchumi wa Tanzania na Zambia. Marais, mawaziri na wananchi wote kila siku tunatakiwa kuimarisha ushirikiano wetu,” amesema Hichilema.