Top 6 Watanzania waliong’ara 2022

HomeKitaifa

Top 6 Watanzania waliong’ara 2022

Kama hatua za binadamu zinavyopishana pale atembeapo  ndivyo maisha ya binadamu yalivyo. Wakati mmoja akienda mbele mmoja hubaki nyuma na Waswahili wakatutungia  msemo wa ‘kuimba kupokezana’.

Wapo ambao hawakuuanza mwaka 2022 kwa kishindo lakini wanaumaliza kwa vifijo na nderemo na wapo waliouanza kwa makeke na wanaumaliza kwa huzuni.Makala haya yanaangazia baadhi ya watu ambao wameibuka vinara kwa katika maeneo mbalimbali kwa mwaka 2022 ilihali hawakutarajiwa wala kutegemewa kuwa watakuwa maarufu na kupata mafanikio haya.

Licha ya kuwa mafanikio waliyoyapata yameboresha maisha yao lakini pia yanatoa ujumbe kwa watu wengine kuhusu uvumilivu na kuzipigania ndoto katika maisha.

1. Karim Mandonga

Nchini Tanzania jina la mwana masumbwi huyu siyo geni kwa masikio ya watu. Tambo zake ambazo huziongea kabla na baada ya pambano imekuwa ni kivutio kikubwa kwa wapenzi wa ndondi na hata wale wasiofuatilia mchezo huo wamejikuta wanaanza  kuupenda.

Bondia Mandonga a.k.a Mtu Kazi alianza kujipatia umaarufu Julai mwaka 2022, wakati  akijiandaa kupigana na bondia Shaaban Kaoneka. Pambano hilo lilifanyika Julai  30 mkoani Ruvuma.  Mandonga alipoteza pambano hilo kwa kupigwa raundi ya nne.

Kutokana na tambo nyingi alizotoa kabla ya pambano hilo, watu wengi walikuwa wakisubiri kwa hamu ushindi wake lakini ikawa tofauti. Hiyo ndiyo ikawa karata yake ya kupata umaarufu mkubwa kwa Watanzania.

Dili za hapa na pale na kualikwa katika shughuli mbalimbali hazikupita mbali naye. Huenda anaumaliza mwaka 2022 kwa kicheko zaidi.

Kauli zake kama ‘umedandia mtumbwi wa vibwengo’, ‘ndoige’, zimekuwa maarufu na zinatumika hata katika michezo mingine kama mpira wa miguu.

Mwaka 2022 unaisha vizuri kwa bondia huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye anapata umaarufu katika umri ambao wengi huwa wanastaafu.

Umaarufu wake umethibitika siyo tu kwa kuwafanya watu waufuatilie mchezo wa ngumi bali kwa sasa anatumika na wafanyabiashara kama balozi wa kutangaza bidhaa zao.

2. Majaliwa Jackson

Kama ulikuwa unawaza waliotunga msemo wa kufa kufaana walikuwa wanawaza nini basi mtazame Majaliwa Jackson. Mvuvi kutoka Bukoba ambaye aligeuka kuwa shujaa wa Taifa baada ya kufanikisha kuufungua mlango wa ndege iliyopata ajali ziwani  na kuokoa maisha ya watu zaidi ya 20.

Novemba 6 mwaka huu, ndege ya Shirika la ndege la Precision Air yenye namba PW 494 ilianguka katika Ziwa Victoria umbali wa mita 100 kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Bukoba ikiwa imetokea jijini Dar es Salaam.

Ndege hiyo ilikuwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, wahudumu wawili na marubani wawili, ambapo Majaliwa na wenzake walifika eneo la ajali dakika tano tu baada ya ndege kuanguka na kuanza shughuli za uokozi.

Majaliwa alipoteza fahamu baada ya kujeruhiwa wakati akiendelea na shughuli za uokozi na kukimbizwa hospitali. Rais aliagiza ajiunge na Jeshi la Zimamoto na Uokozi ili apate mafunzo zaidi. Alitangazwa kuwa shujaa wa Taifa na kutambulishwa bungeni.

Labda ndege isingepata ajali, Majaliwa asingejiunga na Jeshi la Zimamoto na Uokozi kama ilivyoelekezwa. Achilia mbali umaarufu, fedha pamoja na zawadi alizopewa kutokana na tukio hilo, kufa kufaana Majaliwa ameng’ara mwaka 2022.

3. Florian Massawe

Kutoka kuwa fundi gereji mpaka ubilionea. Sikuhamasishi kucheza michezo ya kubashiri ila ndivyo kijana Florian Massawe alivyojikuta bilionea baada ya kucheza mchezo huo kwa muda wa miaka mitano.

Tangu mwaka 2017 amekuwa akibashiri mpaka Mei 16 mwaka huu alipotangazwa na kampuni ya kubashiri ya Sportpesa kuwa ameshinda Sh1.2 bilioni.

Mei 18, 2022, aliwasili katika ofisi za Sportpesa akitumia usafiri wa ndege aina ya helikopta ambapo alikabidhiwa rasmi mfano wa hundi ya Sh1.2 bilioni.

Massawe (36) ambaye ni fundi gereji kutoka Kiluvya mkoani Pwani amekuwa bilionea baada ya kubashiri kwa usahihi mechi zote 13 za ligi mbalimbali duniani ambapo Serikali ilipata kodi ya Sh 188 milioni.

4. Masoud Kipanya

Aprili 2, 2022, mchoraji wa katuni nchini Tanzania ambaye pia ni mtangazaji wa televisheni na redio aliviteka vyombo vya habari ulimwenguni mara baada ya kuzindua gari yake ya umeme aliyoipa jina la Kaypee Motor.

Gari hilo lenye uwezo wa kubeba kilogramu 500, linatumia nishati ya umeme ambayo huchajiwa kwa muda wa saa sita kabla ya kutumika.

Ingawa Kipanya tayari ni mtu maarufu kutokana na shughuli zake za uchoraji na utangazaji, kutengeneza gari kumemfanya awe gumzo zaidi kutokana na namna vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilivyoripoti tukio hilo.

Mashirika ya kimataifa kama Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), China Global Television Network (CGTN) ni miongoni mwa mashirika yaliyoripoti habari hiyo kwa ukubwa.

Kwa sasa Kipanya anaendelea na uzalishaji wa gari zake ambapo alinukuliwa akisema uhaba wa fedha ni miongoni mwa mambo yanayo punguza kasi ya uzalishaji ingawa anatarajia kuuza gari moja au mbili kabla ya mwaka 2022 kuisha.

5. Zuhura Othman Soud  (Zuchu)

Tanzania imebarikiwa kuwa na wasanii wengi wa kike ambao wanafanya vizuri kwa nafasi zao lakini Zuchu ni miongoni mwa wasanii ambao wamefanya vizuri zaidi kwa miaka miwili mfululizo tangu alipotambulishwa mwaka 2020.

Mafanikio yake yamedhihirika kwa kuwa msanii wa kike mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa Youtube (milioni 2.4 ), aidha ndiye msanii wa kike aliyesikilizwa zaidi katika mtandao wa kusikiliza muziki wa  Boomplay.

Mwaka 2022, ameachia nyimbo kadhaa ambazo zimefanya vizuri ndani na nje ya nchi ikiwemo “Kwikwi”, “Jaro”, “Fire” aliomshirikisha msanii Diamond Platnumuz pamoja na “Love” aliomshirikisha msanii kutoka Nigeria Adekunle Gold

Mafanikio yake yameenda nje ya mipaka ya Tanzania kwa kutwa tuzo ya msanii bora wa kike Afrika Mashariki akiwashinda Nandy na Maua Sama, Femi One, Sanaipei Tande na Jovial kutoka Kenya, Sheebah Karungi na Winnie Nwagi wa Uganda.

Zuchu amekuwa chachu ya kuongeza ushindani kwa wanamuziki wa kike nchini Tanzania pamoja na kukuza soko la muziki wa Tanzania nje ya nchi.

6.Gibson Kawago 

Ukionacho wewe taka, kwa mwingine ni fursa . Hivi ndivyo taka za kielekitroniki hususani kompyuta zilizoharibika zilivyobadili maisha ya kijana Gibson Kawago na kumuingiza kwenye ulimwengu wa ubunifu.

Kawago ni mhandisi wa umeme kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) alipata wazo la kutunza mazingira kwa kuzirejeleza betri mwaka 2019 alipokuwa mwaka wa kwanza chuoni akitokea mkoani Iringa.

Gibson aliamua kupunguza athari hizi za mazingira  zitokanazo na mabetri ya kompyuta mpakato kwa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo  vitunza umeme (power bank), taa za umemejua na vitunza betri (battery pack).

Kukosekana kwa nishati ya umeme kijijini kwao kulimsukuma Kawago  kubuni njia mbadala za kupunguza tatizo hilo na kuhakikisha watu wanapata nishati ya umeme mbadala.

Umoja wa Mataifa (UN) unamtambua kama mjasiriamali wa mabadiliko ya tabianchi ambaye pia ni miongoni mwa mabalozi 17 wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) waliochaguliwa na UN kati ya vijana 5,400 kutoka nchi 190.

Kawago sasa ameingia katika orodha ya wajasiriamali 15 barani Afrika wanaotumia teknolojia kusaidia kuhifadhi mazingira, elimu na afya watakaowania tuzo ya vijana wa Afrika wahandisi wenye ubunifu itakayotolewa mwaka 2023

 Mshindi  wa tuzo hiyo atajinyakulia paundi 25,000 za Uingereza sawa na Sh71.3 milioni za Tanzania.

error: Content is protected !!