Wabunge wa Uganda waliokuja kutembelea miundombinu ya nishati nchini wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Maendeleo ya Nishati na Mdibi, Dkt. Peter Lokeris wamesema wamevutiwa na namna Tanzania inavyotumia gesi katika kusambaza umeme.
Walisema hayo baada ya kutembelea kituo cha kupokelea gesi Kinyerezi na Mradi wa kufua umeme Kinyerezi I na II uliopo Dar es Salaam kujionea wanavyosimamia na uzalishaji wake kwa taifa.
“Tumeona wanavyoendesha umeme, gesi Tanzania inakua na inaweza kusambaza hata kwa Bara la Afrika, tumejifunza mengi yatakayotusaidia katika ushirikiano wetu,”alisema Dkt. Lokeris.
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini wa Tanzania, Felschemi Mramba alisema mojawapo ya sababu za msingi za ziara hiyo ya wabunge wa Uganda ni kujifunza miundombinu ya gesi, ikizingatiwa makubaliano yaliyopo ya kujenga bomba ka gesi baina ya nchi mbili.
Alisema Rais Samia Suluhu na Yoweri Museveni walikutana Kampala na kuzungumza jinsi gani ya kujenga bomba la gesi.
“Tayari tulishasaini na tunajiandaa kufanya tathmini ya kujenga bomba hilo. Kamati hiyo ya Uganda imesema ingependa kuona jinsi gani gesi hiyo inatumika kujenga umeme na kutumika kwenye viwanda,” alisema Mramba.